Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kampuni za kimataifa kutoka mataifa zaidi ya 22 mduniani zimeshiriki katika maonyesho ya mafuta na gesi.

Maonyesho hayo yanafanyika kwa mara ya 25 yakihusisha makampuni yanayojishughulisha na masuala ya nishati ya gesi na mafuta.

Uzinduzi wa maonyesho hayo ulifanyika hapo jana katika ukumbi wa diamond jubilee ambapo yalifunguliwa mkurugenzi kutoka mamlaka ya maeneo maalum ya kiuchumi (EPZA).

Akizungumza mara baada ya ufunguzi wa maonyesho hayo mkurugenzi huyo wa uhamasishaji na uwezeshwaji kutoka mamlaka ya maeneo maalum ya kiuchumi, Ndg: James Maziku amesema kuwa kupitia maonyesho hayo ni miongoni mwa rafiki zaidi katika jitihada za kuvutia wawekezaji kwani walioshiriki ni kampuni kutoka zaidi ya mataifa 22 duniani kote na asilimia kubwa ni nchi kutoka nnje mwa bara la Afrika.

“Maonyesho kama haya ni njia rafiki na rahisi yenye gharama nafuu katika kuvutia uwekezaji, mnaweza mkatambua walioshiriki hapa ni zaidi ya mataifa 22 ambayo ni kutoka sehemu mbalimbali na nyingi ni kutoka nnje ya Afrika.

Katika mnyororo wa thamani wa sekta ya mafuta na gesi kuna bidhaa nyingi ambazo zinahitaji teknolojia ya hali ya juu na aidha kuzalishwa hapa nchini na kuitumia nchi hii kama kitovu cha uzalishaji na usambazaji katika masoko yaliyoko karibu.”

Aidha mkurugenzi huyo ameongeza pia kwa kusema kuwa sasa ni wakati sahihi wa kupanua uwekezaji kwa kuwa na mataifa mengi yanayovutiwa kuwekeza nchini kuliko kutegemea taifa moja katika kuchochea uwekezaji.

“Sasa ni wakati muafaka wa kupanua uwekezaji kwa na mataifa mengi tunayoyavutia kuliko kulitegemea taifa moja katika kuchochea uwekezaji nchini” Alisema.

Kwa upande mwingine pia waandaji wa maonyesho hayo kampuni ya expo kupitia mkurugenzi wake wa kanda ya Afrika mashariki Duncan Njage ametoa rai kwa watanzania kujitokeza katika maonesho hayo yanayoendelea kujionea na kupata elimu juu ya utumiaji wa nishati ya gesi na mafuta.

“Tunawasihi watanzania kutembelea maonesho haya kwani kuna makampuni mengi kutoka mataifa makubwa hivyo wataweza kujionea na kupata elimu juu ya utumiaji wa nishati ya gesi na mafuta.” Alisema.

Maonesho hayo yanaoendelea jijini Dar es salaam yanatarajiwa kuhitimika rasmi oktoba 25 mwaka huu.