Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza limemkamata dereva wa gari lenye namba za usajili (T 458 DYD) aina YUTONG BUS kampuni ya Asante Rabi, Shedrack Michael Swai (37), aliyeendesha gari kwa uzembe na kusababisha ajali iliyosababisha vifo vya watu nane, majeruhi zaidi ya 30 na uharibifu wa vyombo.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, DCP, Wilbrod Mutafugwa imeeleza kwamba Oktoba 22, 10, 2024 majira ya saa 11:30 jioni huko wilaya ya Misungwi askari wa usalama barabarani pamoja na askari wengine waliokuwa katika jitihada za kumtafuta dereva huyo walifanikiwa.
Jeshi la Polisi pia linamshikilia dereva mwezake aitwae Karimu Auni (40) mkazi wa Arusha ambaye ni dereva msaidizi wa dereva aliyekuwa akiendesha gari wakati wa ajali, mtakumbuka kwamba utaratibu uliowekwa na serikali mabasi ya masafa marefu yanatakiwa kuendeshwa kwa zamu na madereva wawili ili kuepuka uchovu unaoweza kusababisha ajali.
“Jeshi la Polisi linaendelea kumuhoji dereva huyo Shedrack Michael Swai na hali yake ya kiafya ni mzima hajapata jereha lolote katika ajali hiyo, utaratibu wa kisheria unaendelea kukamilishwa na baada ya uchunguzi jalada litapelekwa kwa mkuu wa mashtaka mkoa kwa ajili ya taratibu zingine za kisheria.”
Katika taarifa hiyo Kamanda Mutafungwa pia ametoa wito kwa madereva wote wanaoendesha vyombo vya moto kuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.