Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

WATUMISHI Housing Investment (WHI) imetunukiwa tuzo ya ‘Nyumba za gharama nafuu zaidi Afrika’ iliyotolewa na Taasisi ya Mikopo ya Nyumba Afrika inayotambuliwa na Umoja wa Afrika.

Tuzo hiyo imetolewa katika mkutano Mkuu wa AUHF mwaka 2024 uliofanyika Zanzibar hivi karibuni, WHI iliibuka kinara kutoka kwa taasisi mbalimbali zinazohusiana na sekta ya makazi kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 23, 2024 Mkurugenzi Mtendaji wa WHI, Dkt. Fred Msemwa amesema tuzo hiyo ya heshima inatambua jukumu la WHI katika kuwezesha umiliki wa nyumba kwa watu wa kipato cha chini na kati nchini Tanzania.

“Juhudi zilizofanywa na WHI katika kuleta suluhisho la njia nafuu za malipo za nyumba ikiwemo malipo endelevu yanayolipwa kipindi cha ujenzi bila riba pamoja na utaratibu wa mpangaji mnunuzi ambavyo vilitajwa kama sababu kuu za ushindi huu.

“Njia hizi zimeleta unafuu mkubwa sana kwa watu wanaotamani kumiliki
nyumba. Nyumba za WHI zinauzwa kwa bei nafuu kwa kati ya asilimia 10 hadi
ikilinganishwa na nyumba kama hizo kwenye soko, huku bei ya kununua nyumba ikianzia Sh. milioni 38,” amesema.

Amefafanua kuwa, bei hizo pamoja na njia nafuu za malipo zimewasaidia Watanzania wengi kufikia ndoto zao za kumiliki nyumba.

“Tuzo hii pia inasherehekea kipindi maalum kwa WHI, kwani inatimiza miaka 10 ya bunifu na ongozi katika sekta ya Makazi. WHI inakuwa taasisi ya kwanza chini na Afrika Mashariki kupokea Tuzo hii ya heshima.

“Tuzo za AUHF zinatambua michango thabiti ya kuendeleza sekta ya makazi barani Afrika. Ushindi wa WHI ulitokana na utekelezaji wake wa kipekee katika kubuni na kutekeleza miradi ya numba yenye gharama nafuu zaidi a hivyo kuleta unafuu kwa wanunuzi ikiwalenga watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii,” amesema.

Ameongeza kuwa, Shirika hilo muhimu linalounganisha wadau wa makazi barani Afrika kwa zaidi ya miaka 40, linawezesha washirika wake kuendeleza fumbuzi zaidi wa makazi ya bei nafuu. Ahadi ya WHI ya kupunguza gharama za makazi na kutoa njia mbadala za malipo ilionekana kama hatua kubwa kuelekea kufikia maono haya.

“Tuzo hii ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali kupitia Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa umma na Utawala Bora katika kuwawezesha wananchi wake kupata makazi nafuu.

“Watumishi Housing Investments ni taasisi ya umma chini ya Ofisi ya Rais UTUMISHI yenye jukumu la undelezaji wa milki na usimamizi wa mifuko ya uwekezaji wa pamoja. WHI inasimamia mifuko mivili yaani Mfuko wa Nyumba na Mfuko wa Faida Fund,” amesema.