Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) limesema hadi sasa watu 90,000 wamesajiliwa kwenye Kazidata ya Programu Maalum ya Imarisha Uchumi na Mama Samia (IMASA) yenye lengo la kuinua uchumi wa Watanzania yakiwemo makundi maalum.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Uwezeshaji wa Baraza hilo kwenye kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika leo Oktoba 22, 2024 Jijini Dar es Salaam.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bi. Beng’i Issa  akizungumza alipokuwa akifungua rasmi kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika leo Oktoba 22, 2024 jijini Dar es Salaam.

Mwakatobe amesema kuwa programu ya IMASA inatekelezwa kwenye mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na mikoa mitano ya Zanzibar, na kwamba kwa sasa wapo kwenye hatua ya kwanza ya programu hiyo na tayari wametembelea mikoa 24 ya Tanzania Bara na utekelezaji wake unatarajia kuanza mwaka wa fedha 2024/2025.

Tumejadiliana na viongozi wa mikoa kuhusu shughuli za kiuchumi zinazopatikana kwenye maeneo yao ambazo zitawanufaisha wananchi. Tunaibua vipaumbele ambavyo vitagusa makundi mbalimbali, akinamama, vijana na walemavu, “ amesema Neema.

Ameongeza kuwa mara baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza, wataingia kwenye awamu ya pili ambayo itahusisha upelekaji wa fursa na programu kulingana na shughuli za kiuchumi walizoziona kwenye mikoa waliyotembelea. “Programu hii ya IMASA inazitambua Programu nyingine zilizopo nchini ikiwemo BBT.”

Awali akizungumza wakati akifungua kikao hicho, Katibu Mtendaji wa NEEC Bi. Beng’i Issa, amesema kuwa Baraza hilo limekuwa likichukua hatua mbalimbali kuwafikia wananchi kote nchini kuwapa elimu ili kufahamu fursa mbalimbali zilizopo za uwezeshwaji kiuchumi na mitaji. 

Aidha amesema kuwa pamoja na maeneo mengine pia wanatoa elimu ya kuimarisha mfumo wa elimu ya ujasiriamali na mazingira ya uwekezaji.