Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Babati

Migogoro baina ya wanyamapori na binadamu imepata tiba baada ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuja na mfumo wa usimamizi wanyama wakali na waharibifu (PAIS) katika Wilaya ya Babati,Mkoa Manyara.

Katika mfumo huo, unawezesha wananchi kutoa taarifa haraka za uwepo wa wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo yao na zitawafikia maafisa wa wanyamapori na kuchukuliwa hatua za haraka.

Mkuu wa Wilaya ya Babati,Emmanuela Kaganda akisalimiana na Meneja wa Taasisi ya Chem Chem,Clever Zulu baada ya kufungua mafunzo ya mfumo wa PAIS wa kudhitibi migogoro ya binaadamu na wanyamapori

Mfumo huo pia unarahisisha kuandika madai ya uharibifu wa wanyamapori,Uhakiki na malipo ndani ya muda mfupi tofauti na miaka ya nyuma.

Akifungua mafunzo ya viongozi wa Serikali katika eneo la Ikolojia ya Manyara-Tarangire, Mkuu wa Wilaya ya Babati Emanuela Kaganda alisema mfumo huo ukitumika vizuri utapunguza sana migogoro baina ya wanyamapori na Binaadamu wilayani Babati.

“Nawapongeza sana Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuja na mfumo huu ambao unawezesha kudhibitiwa uharibifu wa mazao ama madhara ya wanyamapori kabla haujatokea na nawapongeza chemchem kwa kuwezesha kufanyika mafunzo haya “alisema.

Kaganda alisema mfumo huo ,unarahisisha pia mchakato wa kutoa mkono wa pole kwa wananchi watakao pata athari za wanyama .

Kaganda alisema, mfumo huo utakuwa na faida kubwa kama viongozi wakiujua na hivyo kuwaelimisha wananchi vijijini.

“Serikali inataka migogoro baina ya wanyamapori na binaadamu imalizwe na tunaimani mfumo huu itasaidia sana kupunguza migogoro hii”alisema

Akitoa mafunzo ya mfumo huo, Afisa TEHAMA mwandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Kelvin Mtei alisema mfumo huo ni rahisi sana na utakuwa na manufaa makubwa.

MkuuMkuu wa wilaya ya Babati,Emmanuela Kaganda akifungua mafunzo ya mfumo wa PAIS wa kudhitibi migogoro ya binaadamu na wanyamapori

Mtei alisema mfumo huo umeunganishwa na Mkurugenzi wa Wanyamapori, Mamlaka ya usimamizi wanyamapori(TAWA) ,Shirika la hifadhi za Taifa(TANAPA) Wakala wa misitu (TFS) na Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro(NCAA).

“Mfumo huu unawezesha mwananchi kutuma taarifa kupitia simu ya mkono kwa haraka na hivyo kudhibitiwa wanyamapori”alisema

Afisa Wanyamapori kutoka wizara ya Maliasili na Utalii,Hamisi Ashery alisema mfumo huo ni rafiki na utawezesha sasa malipo ya vifuta machozi kutolewa kwa wakati.

“Mfumo huu ukiingia unaonesha kila jambo ambalo unahitaji na unapunguza sana kazi za maafisa wanyamapori,maafisa kilimo ma wengine kufanya tathmini za uharibifu na kuandika madai”alisema

Afisa Ujirani mwema katika hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara,Maingo ole Kili alisema mfumo huo ni suluhu ya migogoro baina ya wanyamapori na binaadamu

Mafunzo ya mfumo huo yamedhaminiwa na taasisi ya Chemchem association ambayo imewekeza shughuli za uhifadhi na Utalii katika eneo la hifadhi ya jamii ya wanyamapori ya Burunge wilayani Babati,mkoa Manyara.