Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, ni wazi safari yake ya kupoteza wadhifa huo imeiva. Msomaji naamini umefuatilia kwa karibu sakata la kuondolewa madarakani kwa huyu Naibu wa Rais, ambaye bado anaamini mahakama itamsaidia. Inahitaji kuwa na moyo wa mwendawazimu kuamini kuwa mahakama itamwokoa Gachagua.
Sitanii, naamini umefuatilia kwa karibu kilichomtokea Gachagua huko Kenya. Gachagua ambaye mwaka 2022 aliunganisha nguvu na aliyekuwa Naibu Rais wa wakati huo, Dk. William Ruto, kupambana dhidi ya Mzee wa ODM, Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta katika harakati za kugombea urais, wakati huo alikuwa na nidhamu. Natumia neno nidhamu kwa makusudi, kama utakavyoona hapa chini.
Wawili hao, Gachagua na Ruto waliunganisha nguvu na kumwangusha Mzee Raila. Mwaka wa kwanza ulikuwa wa sherehe kila kona nchini Kenya.
Hata hivyo walianza kuona dalili mbaya baada ya Rais Ruto kufuta ruzuku ya mafuta. Bei ya petroli nchini Kenya ikawa juu kuliko nchi zote zinazoizunguka. Wakenya wakaanza kununua mafuta kwa magendo kutoka Tanzania.
Kama hiyo haitoshi, bei ya unga nayo ikawa inazidi kupanda. Wananchi wakaanza kulalamika. Mtakumbuka Kenya kutokana na mzigo mkubwa wa madeni, mwaka huu Serikali ya Rais Ruto ilipeleka bungeni muswada wa kuongeza kodi katika maeneo mbalimbali. Gachagua katika hatua hii akaanza kusahau uwajibikaji wa pamoja. Hali ya maisha ikazidi kuwa ngumu nchini Kenya. Vijana wa Gen-Z wakaandamana barabarani.
Maandamano ya Gen-Z yaliilazimu Serikali ya Rais Ruto kuvunja Baraza la Mawaziri. Katika hatua hii, taifa la Kenya lilikuwa na mgawanyiko mkubwa. Upinzani ulionekana kuungwa mkono. Katika hatua hiyo, ikabidi Rais Ruto ameze maneno yake. Awali alikuwa na msimamo kuwa “Hakuna nusu mkate”, lakini baada ya maandamano akazungumza na Raila, kisha serikali ya Rais Ruto ikatoa nafasi kwa viongozi wa upinzani kuwa mawaziri.
Sitanii, Gachagua hakulipenda hili. Akaanza kutoa kauli zenye ukakasi. Akaenda mbali akasema yeye ndiye ana mtaji mkubwa kwenye serikali ya Rais Ruto.
Akasema bila watu wa ‘Mlima’, akimaanisha Wakikuyu kutoka Mlima Kenya wasingeipigia kura serikali ya Rais Ruto, isingeshinda. Akaenda mbali zaidi akamwomba radhi Rais Uhuru Kenyatta, ambaye alikataa kumuunga mkono Ruto akisema anavyomfahamu hastahili kuwa Rais.
Gachagua akailinganisha serikali na kampuni, akisema mwenye hisa nyingi ndiye anayestahili kupewa maziwa mengi ng’ombe akizaa. Kama hiyo haitoshi, akaanza kutoa lugha za ubaguzi ambazo zinaonyesha makabila ya kutoka Mlima Kenya yana thamani kuliko watu wengine. Serikali za Majimbo, ikiwamo ile ya Nairobi, akaziona hazifai tena.
Wiki tatu zilizopita nilikuwa Nairobi. Nilipata fursa ya kuzungumza na watu wa kada mbalimbali, kuanzia katikati ya jiji hadi Kibera. Kubwa nililoliona linawakera mno Wakenya, ni ukabila. Utashangaa msomaji. Wakenya vijana wenye miaka kuanzia 40 kurudi chini, wanakataa ukabila. Kubwa wanasema wanajifunza kutoka Tanzania tunavyoishi kama ndugu.
Gachagua, mwenye umri wa miaka 59 kwake yeye hilo hakuliona kama tatizo kurejesha lugha za kibaguzi. Lakini jambo jingine, Gachagua alianza kuonyesha dharau kubwa kwa Rais Ruto. Aliamini katika Bunge wapo aliowasaidia kupata ubunge, hivyo wangemuunga mkono katika mapambano yake na Rais Ruto.
Sitanii, kumbe Gachagua alichagua mkondo usio sahihi. Hakujua kuwa wanadamu karibu wote, wanajisikia salama zaidi wakijihusisha na mamlaka. Wapo watu wanaojiuliza iwapo mtu ana akili timamu, anapopingana na Rais wa nchi si kwa hoja, bali kwa masilahi binafsi akiamini kuwa anaweza kumwangusha kisha akawa yeye.
Hapana shaka katika kukosea hesabu, Gachagua baada ya kusoma Katiba ya Kenya akaona inasema Rais akivuliwa madaraka Naibu Rais anaapishwa kuwa Rais, akaanza kumchimba Ruto, akidhani akiondoka yeye anakuwa Rais. Ni katika hatua hii, mdomo umemponza. Hata aliowatarajia wamwokoe kwenye Bunge na Seneti, wakamchinjia baharini.
Ni wazi sasa amekwishavuka hatua mbili. Bungeni na kwenye Seneti amekwishapoteza wadhifa wa Naibu Rais. Amekimbilia mahakamani. Hatari iliyopo, hata huko mahakamani anakwenda kupoteza kesi hii. Nasema anakwenda kupoteza kesi hii, maana hayo maneno ya ukabila hakani kuyatamka. Kwa hakika anakwenda kuyathibitisha mahakamani, na kurahisisha hatua ya kumtia hatiani.
Sitanii, angebaini kuwa kumbe sasa tayari Rais Ruto hawako pamoja tena.
Amekwisha kumteua Waziri wa Mambo ya Ndani, Abraham Kithure Kindiki, kuwa Naibu Rais, na Bunge limempitisha kwa kishindo, angefunga breki. Kura zote zimemkubali Kindiki. Kinachosubiriwa ni hizo siku 14 ilizosema mahakama kwa mujibu wa Katiba, ambazo sasa naamini wanakwenda kubariki uamuzi wa Bunge na Seneti.
Wakati nahitimisha makala hii, naomba kusema viongozi wote hata katika nchi yetu wanapaswa kuheshimu dhana na msingi wa uwajibikaji wa pamoja. Serikali inapofanya uamuzi, nyote mliomo katika Baraza la Mawaziri ni uamuzi wenu nyote kwa pamoja.
Hakuna waziri anayepaswa kutoka nje akasema uamuzi ule ni wa Rais au Makamu wa Rais au Waziri Mkuu au Naibu Waziri Mkuu, yeye aliupinga. Gachagua ameyafanya yote hayo!
Pia ni onyo kwa mawaziri, watendaji au viongozi ndani ya vyama wanaowadharau wenyeviti wao au viongozi wa juu bila kujali ni chama cha upinzani au chama tawala.
Mfano leo mwanachama yeyote kuamka asubuhi akapingana na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, hadharani bila nguvu ya hoja, anakuwa akitoboa jahazi la CHADEMA.
Tumewaona wengi waliothubutu, ni ama wameanzisha vyama vyao, au wamehamia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Naamini hata kwenye Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, akitokea mtu wa kumdharau kwa mkondo wa Gachagua, tumeshuhudia waliothubutu walivyoliwa vichwa.
Ni wazi uwajibikaji wa pamoja ni muhimu. Viongozi katika serikali wanapaswa kuzungumza lugha moja, ukifungua mdomo kwa masilahi binafsi na si ya umma, yaliyomkuta Gachagua hautayakwepa.
0784404827