Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha
Naibu Kamishna wa Ardhi kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wilson Luge amewataka vijana kuzingatia suala la ongezeko la idadi ya watu wakati wa kupanga matumizi bora ya ardhi.
Kamishna Luge amesema haya wakati akifungua Kongamano la nne la Kimataifa la vijana na Utawala wa Ardhi barani Afrika (CIGOFA4) lililoanza leo jijini Arusha.
Amesema idadi ya watu kwa nchi zote za Afrika zinaendelea kuongezeka wakati ardhi inayotegemewa ni ile Ile hivyo kuwataka washiriki wa kongamano hilo kuhakikisha mikakati hiyo inaendana na ongezeko la idadi ya watu.
“Kwa mfano hapa nchini kwetu Tanzania kwa kipindi cha mwaka 2007 kama kila mwananchi angepewa ardhi angepata hekta 7.4, lakini leo hii tukisema kila mtu apewe ardhi kulingana na idadi ya watu kwa ya mwaka 2022 kila mwananchi atapata hekta 1.5”
“Hii inaonyesha ardhi haiongezeki wakati idadi ya watu ikiongezeka, ndiyo maana nawasisitiza vijana washiriki katika mipango wasiwaachie wazee pekee ili hata kwenye utekelezaji wawepo kwa kuwa wao ndiyo nguvu kazi ya Taifa” amesema Luge.
Mkurugenzi wa Jumuiya ya Vijana kwa Ajili ya Ardhi barani Afrika (YILAA Afrika) Innocent Antoine amesema katika Kongamano hilo watapitia sera za ardhi kutoka nchi mbalimbali barani Afrika ili kuona kama zinatoa nafasi kwa vijana kumiliki ardhi na kisha kutoka na mapendekezo.
“Kupitia political dialogue (mazungumzo ya kisiasa) tutaangalia sera za nchini mwetu kuona zinasemaje kuhusu vijana na umiliki wa ardhi ili tuje na maazimio ya pamoja” amesema Antoine
Kwa upande mwingine Antoine amesema kuna changamoto ya vijana kuuza ardhi wanazopewa hivyo kupitia kongamano hilo watatoa elimu ya umuhimu wa ardhi kwa maendeleo endelevu.
Suzana Tuke kutoka jamii ya kimaasai wilayani Kiteto katika mkoa wa Manyara amesema bado mtoto wa kike kutoka jamii hiyo hawana haki ya kumiliki ardhi.
Amesema kupitia mafunzo atakayopata kutoka katika kongamano hilo ataenda kuelimisha kwa jamii yake.
Sera ya Ardhi nchini Tanzania ya mwaka 1995 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023 imeweka usawa katika kumiliki ardhi kwa maana kila Mtanzania mwenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea ana uwezo wa kumiliki ardhi, chini ya umri huo atamiliki chini ya usimamizi wa mtu mzima.