Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema Mradi wa Utafiti wa Mafuta ghafi na gesi kwenye Bonde la Eyasi Wembere lililopo katika mikoa ya Simiyu, Singida na Arusha utekelezaji wake umefikia asilimia 40.
Mradi huo unaotekelezwa kwa fedha za serikali zaidi ya Sh bilioni 40 ulianza mwaka 2015 ambapo shughuli zinazoendelea kufanyika ni uchukuaji wa taarifa (Data) za mitetemo na kuzichakata ili kuwa na uhakikia wa uwepo wa mafuta au gesi.
Akizungumza mbele ya wajumbe wa Bodi ya TPDC waliotembelea mradi huo jana, Kaimu Meneja wa Utafutaji kutoka TPDC Simino Nyarusi alisema kuwa shughuli za utafiti zinazofanyika katika bonde hilo, zinatekelezwa kwenye maeneo mawili ambayo ni eneo la nchi kavu na eneo la ziwani ndani ya Ziwa Eyasi.
Alisema katika eneo la nchi kavu wamefanikiwa kufikia asilimia 40 ya utafiti huo, ambapo alibainisha kuanza kuonekana kwa viashiria mbalimbali ambavyo vimetoa matumaini makubwa ya uwepo wa mafuta na gesi.
“ Utafiti huu ulianza toka mwaka 2015, tumepitia hatua mbalimbali, ambapo kwa hatua hii ambayo tunaendelea kutekeleza, tumeanza kuona mafanikio makubwa, tuko asilimia 40 ya utafiti wetu na tumeanza kuona viashiria vikubwa vya uwepo wa mafuta,” alisema Nyarusi.