Na Zulfa Mfinanga, Jamhuri Media,
Arusha.
Mkutano wa nne wa Kimataifa wa Vijana na Utawala wa Ardhi barani Afrika (CIGOFA4) unatarajiwa kufanyika kwa siku nne kuanzia kesho jijini Arusha wenye lengo la kuharakisha haki za vijana katika ardhi.
Mkutano huo ulioandaliwa na Jumuiya ya Vijana kwa Ajili ya Ardhi barani Afrika (YILAA) utawaleta kwa pamoja wadau mbalimbali wa kitaifa na kimataifa ili kuendeleza ajenda ya utawala wa ardhi wa vijana katika bara la Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa leo, Mkurugenzi Mkuu wa YILAA Afrika Innocent Antoine amesema CIGOFA4 inalenga kuwawezesha vijana kwa kutoa jukwaa la mazungumzo, kubadilishana maarifa na ushirikiriano katika masuala muhimu yanayohusiana na haki ya ardhi za vijana, mabadiliko ya tabia nchi na vijana pamoja na maendeleo endelevu.
“Washiriki zaidi ya 500 kutoka Afrika na kwingineko ikiwa ni pamoja na vijana wanaoishi pembezoni, mamlaka za jadi, wawakilishi wa serikali pamoja na wataalamu wa kimataifa watakuwepo ili kuhakikisha malengo ya CIGOFA4 ya kuwezesha vijana, kubadilisha maarifa pamoja kuunda sera ya afikiwa” amesema Antoine.
Antoine amesema mbali na majadiliano juu ya haki za ardhi za vijana lakini washiriki watapata fursa ya kujadili usalama wa chakula, uvimbuzi katika kilimo, makazi na ramani za ardhi.
Ameongeza kuwa kuwakuwepo na maonyesho ya hadithi za mafanikio kupitia miradi iliyofanikiwa kama vile ushirikiriano wa YILAA na jumuiya za asili, ili kutoa mifano halisi ya athari chanya.
Kwa upande kwake Mkurugenzi wa YILAA Tanzania Augustine Nyakatoma amesema nchi nyingi barani Afrika hazina utaratibu wa kisera wa kummilikisha kijana ardhi na badala yake vijana wengi wanamiliki ardhi kwa mfumo wa kurithi baada ya wazazi wao kufariki.
Nyakatoma amesema kupitia kongamano hilo vijana watajadili changamoto za kumiliki ardhi na kisha kuja na suluhu.
Kuhusiana na nafasi ya mwanamke na mtoto wa kike katika utawala wa ardhi, Deborah Oyugi ambaye ni mratibu wa nchi zinazozungumza lugha ya kujitolea amesema kongamano hilo litawajengea uwezo kundi hilo ili kuhakikisha sauti zao zinasikika na michango yao inatekelezwa.
“Linapokuja suala la mwanamke na mtoto wa kike tunapaswa kuhakikisha tunalifuatilia hadi utekelezaji wake kwa sababu nchi nyingi za Afrika zina sheria na sera nzuri za wanawake na watoto wa kike lakini utekelezaji wake hauna nguvu ya kisheria” amesema Oyugi.
Mratibu wa Jukwaa hilo Bernard Baha amesema mkutano huo umeandaliwa na YILAA kwa kushirikiana wadau mbalimbali waliwemo Muungano wa Ardhi wa Tanzania (TALA), Umoja wa Afrika (AU), GIZ na wadau wengine ambapo Kauli Mbiu ni, Kuharakisha Haki za Vijana Katika Ardhi.