Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) na Shirika la ujasusi Shin Bet wamethibitisha uwezekano wa kiongozi wa Hamas, Yahya Sinwar, kuuawa katika shambulizi la hivi karibuni la anga lililofanywa Gaza.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israeli, uwezekano wa Sinwar kuuawa umeendelea kuongezeka, lakini bado utambulisho wa walioaga dunia haujathibitishwa rasmi.

Shambulizi hilo lilifanyika wakati vikosi vya IDF vilipokuwa vikifanya operesheni maalum katika Ukanda wa Gaza, ambako walifanikiwa kuangamiza wapiganaji watatu wa Hamas.

Taarifa za awali zinasema kwamba Sinwar anaweza kuwa mmoja wa waliouawa. Hata hivyo, jeshi la Israeli bado linafanya uchunguzi zaidi ili kuthibitisha.

Yahya Sinwar amekuwa kiongozi muhimu wa Hamas na anatuhumiwa kupanga mauaji ya tarehe 7 Oktoba, ambayo yalipelekea vifo vya watu zaidi ya 1,200, wakiwemo Waisraeli na raia wa mataifa mengine.

Katika mashambulizi hayo, zaidi ya watu 250 walitekwa nyara, ambapo 101 bado wanashikiliwa Gaza, huku 48 wakiripotiwa kuuawa wakiwa mateka.

Kwa muda mrefu, Sinwar amekuwa akijificha ndani ya mitaro ya Hamas huko Gaza, na alijulikana kuepuka matumizi ya teknolojia ya mawasiliano, akitegemea wajumbe kumfikishia taarifa.

Israeli imekuwa ikiendeleza operesheni za kumuondoa viongozi wa juu wa Hamas, ikiwemo kuwaua Ismail Haniyeh na Mohammed Deif katika mashambulizi yaliyopita.

Hali bado inaendelea kufuatiliwa huku Israeli ikiendelea na operesheni zake.