Na Hassan Msellem , JamhuriMedia, Pemba

Mabaraza ya vijana yalianza mwaka 1948 nchini Urusi. Lengo la kuanzishwa kwake ni kuwaunganisha vijana wa maeneo mbalimbali ili kutambuana na kuwa wazalendo wa taifa lao hasa pale inapobidi kulitetea dhidi ya adui, ikizingatiwa kipindi hicho dunia ilikuwa inakabiliwa na Vita Kuu ya Pili (WWII).

Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, Salum Issa Ameir, anasema vijana waliojiunga na mabaraza ya vijana katika wilaya zote za Pemba ni 9,308 huku wanaume wakiwa 4,754 na wanawake 4,553 sawa na asilimia 48 ya vijana wa kike waliojiunga.

Kwa upande wa Micheweni, vijana wa kiume waliojiunga ni 1,078 na wanawake ni 952, Wete wanaume ni 1,176 na wanawake ni 1,041, Chake Chake wanaume ni 1,260 na wanawake ni 1,386 na Mkoani wanaume ni 1,240 na wanawake ni 1,174.

Mkaazi wa Wawi, Chake Chake, Ali Omar Juma (28), anasema malengo ya uanzishwaji wa mabaraza hayo ni mazuri lakini mifumo ya uendeshaji wake si rafiki.

Anasema si rafiki kuanzia njia ya upatikanaji wa wanachama na namna yanavyoendeshwa huku akijitolea mfano alishindwa kujiunga na Baraza la Chake Chake kutokana na ‘danadana aliyokumbana nayo kwa kudhaniwa yeye ni mfuasi wa chama cha upinzani.

Nilitamani kujiunga na baraza la vijana lakini nimeshindwa kutokana na uendeshwaji wake, ukisoma sera na malengo ya uanzishwaji ni mazuri lakini yanashindwa kufikiwa.

“Mfumo hautoi nafasi kwa kila kijana anayejisikia kuwa mwanachama ajiunge maana ukiangalia asilimia kubwa ya vijana waliomo kwenye mabaraza hayo ni vijana wa chama tawala, anasema.

Hoja hiyo inaungwa mkono na mkaazi wa Shehia ya Wesha, Chake Chake, Hafsa Maulid Azizi (22), anayesema anasikia kuhusu mabaraza hayo lakini hana taarifa za kutosha.

Mwanafunzi wa Chuo cha Samali Gombani, Hafsa Maulid Aziz, akizungumza katika kikao kimoja cha baraza la vijana.

Tangu nipo sekondari na sasa nipo chuo sijawahi kupata taarifa wala elimu yoyote kuhusu mabaraza ya vijana. Sifahamu wapi zipo ofisi zake wala vipi naweza kujiunga, hapo kweli tutasema mabaraza hayo yapo kwa vijana wote au kwa baadhi tu? Amehoji.

Anawataka viongozi wa mabaraza hayo kutafakari upya mwenendo wake ili yafanye kazi kwa uadilifu kwa ajili ya kuwafikia vijana.

Lengo la kuundwa
Baraza la Vijana Zanzibar limeundwa kwa mujibu wa matakwa ya kisheria yanayoelekeza haja ya kuwajenga vijana kuutambua utaifa wao, umoja, mshikamano na kujiheshimu.

Pia kufanya kazi kama jukwaa na kiungo wakilishi kwa masuala ya vijana, kuwajengea uwezo na kuwafanya wazalishaji katika jamii na kuwakilisha maslahi yao ndani na nje ya nchi.

Baraza hilo ni chombo kinachojitegemea kilichoanzishwa chini ya Sheria namba 16 ya mwaka 2013 na kutiwa saini Juni 30, 2014 na Rais wa Awamu ya Saba wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.

Pemba ina jumla ya wilaya nne za Mkoani, Chake Chake, Wete na Micheweni na zote hizo zina mabaraza ya vijana yanayowalea na kuwafanya kuwa viongozi bora wenye nidhamu, maadili, uzalendo na uthubutu wa kiutendaji katika nafasi mbalimbali.

Sera inasemaje?

Ibara ya 6 ya Sera ya uanzishwaji wake inaeleza usawa wa kijinsia katika mabaraza hayo kwa mujibu wa mgawanyo wa nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya shehia, wilaya hadi taifa.


Mathalani katika usawa huo wa jinsia ni pale kifungu cha pili katika ibara hiyo kueleza kutakuwa na mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa baraza hilo kuanzia ngazi ya wilaya kwa kuzingatia utofauti wa jinsia.

Baraza latoa fursa

Mkaazi wa Majanzi, Micheweni Mkoa wa
Kaskazini Pemba, Saumu Mohammed Said (31), anasema baraza hilo ndilo limemsaidia kupata nafasi mbalimbali za uongozi.

Mwaka 2020, Saumu ambaye kitaaluma ni mwalimu aliteuliwa kuwa Diwani wa Wadi ya Wingwi, Micheweni.

Kabla ya uteuzi huo, yeye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Vijana Taifa-Micheweni, Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kaskazini Pemba kuanzia mwaka 2017 hadi 2022, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wadi ya Sizini na Mjumbe wa Kamati ya Propaganda na Uenezi Wilaya ya Micheweni kupitia CCM.

Kwa asilimia kubwa mchango wa baraza la vijana umeniwezesha kuteuliwa kuwa diwani. Kama nisingekuwa kwenye baraza la vijana nisingeonekana naweza kushika nafasi hiyo na kuifanyia kazi ipasavyo.

Vijana wa kike tunakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo uhaba wa wanawake wanaojiunga na kutakiwa kimapenzi na baadhi ya viongozi na rushwa ya ngono kukatishwa tamaa ya kutokutimiza ndoto zao, anasema.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Mkoani, Ruwaida Mohammed Omar (30), anasema mabaraza yana mchango mkubwa kuwaandaa wanawake kushika nafasi za uongozi kwa kuwapo usawa wa kijinsia pamoja mafunzo mbalimbali ya uongozi.

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Wilaya ya Mkoani, Ruwaida Mohammed Omari, akizungumza katika moja ya vikao vya mabaraza ya vijana.

Mabaraza yana mchango mkubwa kuwaandaa vijana wakike kushika nafasi za uongozi kwa sababu unapokuwa mwanachama au kiongozi wa baraza kuna mafunzo yanayoandaliwa yanakupa mwelekeo wa kuwa kiongozi bora. Hadi sasa nimeshashika nafasi za uongozi zaidi ya nne kutokana na uzoefu niliopata, anasema.

Walezi wa mabaraza

Wakuu wa wilaya ni walezi na wasimamizi wa mabaraza ya vijana wilayani.

Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Mgeni Khatib Yahya ni mlezi wa baraza la vijana wilayani humo. Katika kuhakikisha wasichana na wanawake wanapatiwa fursa ya kujiunga na baraza, anasema ameweka utaratibu wa kukutana nao kila mwaka.

Nikiwa kama mlezi nahakikisha wasichana na wanawake hasa wanaosoma kuanzia sekondari na vyuoni tunawapa elimu na kuwaonyesha faida za kujiunga na tunashukuru mwitikio unaridhisha, anasema.

Kuhusu ubaguzi wa kichama katika mabaraza hayo anasema na kuongeza: Ni kweli hayo malalamiko yapo tangu sijateuliwa kushika nafasi hii tangu mwenyewe niko katika mabaraza lakini ukweli ni kwamba si kwamba vijana wa CCM ndio walengwa.

Haya mabaraza yameanzishwa kwa ajili ya vijana wote wenye sifa ila tu wengi wenye mwamko wa kujiunga ni wa CCM.

Jinsi elimu inavyotolewa

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Mkoani, Abdalla Saleh Issa, anasema njia wanazozitumia kutoa taarifa na elimu kwa vijana ili kujiunga na mabaraza ni mabonanza, mikusanyiko, vikundi vya wajasiriamali, mikutano ya kijamii, siku ya Mwenge wa Uhuru, vipindi vya redio na vipeperushi.

Si kweli kwamba vijana wengi hawana elimu ya mabaraza kwa sababu viongozi wanatumia njia mbalimbali kuitoa na tunawafikia mijini na vijijini, anasema.

Pia katika kuhakikisha usawa wa kijinsia unafikiwa kwenye vyombo vya kutunga sheria na hata nafasi mbalimbali za uteuzi serikalini, Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Pemba, Fat-hiya Mussa Said, anasema wanaendelea na programu za kuongeza idadi ya viongozi wanawake katika vyombo vya uamuzi kama vile Baraza la Wawakilishi na Bunge.

Vyombo vya uamuzi vinaanza usheha na udiwani. Nafasi za uteuzi serikalini kwa mfano kwa sasa tuna Katibu Mkuu Kiongozi wa kwanza mwanamke Zanzibar, RC wa kwanza mwanamke Pemba na yote hayo ni miongoni mwa matunda ya programu zetu,” anasema.

Please follow and like us:
Pin Share