Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Dalaam

Mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Congo, Fiston Mayele amesema mchezaji pekee wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) waliyekuwa wakimuhofia ni Simon Msuva kutokana na uwezo wake mkubwa wa kukimbia eneo sahihi.

Mayele ameyasema hayo baada ya mechi ya Tanzania vs Congo iliyochezwa katika dimba la Mkapa na kumalizika kwa Stars kupoteza kwa mabao (2-0) yaliyofungwa na Meshack Elia.

“Mchezaji kama Msuva, kwa upande wetu ndiye mchezaji ambaye hata Kocha alikuwa ananiuliza kama ataitwa au vipi, kama angekuwa pale na Samatta angetusumbua sana kwa sababu anakimbia kwenye ‘Space’ na Samatta alikuwa analinda mpira vizuri hata mechi ya kwanza amecheza vizuri, kwahiyo sisi tumepata faida kwa sababu Msuva hayupo”

Congo kwa sasa ipo kileleni mwa kundi H wakiwa na pointi 12, na tayari wameshafuzu kwenda AFCON nchini Morocco mwakani huku wakiwa wamebakisha michezo miwili dhidi ya Guinea na Ethiopia.

Taifa Stars inashika nafasi ya tatu katika kundi hilo ikiwa na alama nne, huku wakiwa wamebakisha michezo miwili dhidi ya Ethiopia ugenini na Guinea katika dimba la Mkapa.

Please follow and like us:
Pin Share