Na Happiness Shayo, JamhuriMedia, Arusha

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) ameielekeza menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kubuni mikakati ya kuongeza mapato yatokanayo na Utalii ikiwa ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ametoa kauli hiyo leo Oktoba 16,2024 alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika Ofisi zao zilizopo jijini Arusha.

” Niwapongeze kwa kazi nzuri mnayoifanya lakini Mheshimiwa Rais anataka tuongeze mapato na tubuni mazao mapya ya utalii ” amesisitiza.

Aidha, ameielekeza Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) ihakikishe inatoa ufumbuzi wa changamoto ya magugu vamizi yanayoharibu uoto wa asili ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.

“Natoa siku saba kwa TAFORI waende katika bonde la Kreta na kutoa ufumbuzi wa namna ya kudhibiti mimea vamizi ” amesisitiza Mhe. Chana.

Naye, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utalii, Nkoba Mabula ameitaka mamlaka hiyo kuwa wabunifu, kuangalia namna ya kujitangaza na kubuni mazao mengine ya utalii ili kuiongezea Serikali mapato.

Kikao hicho ni muendelezo wa Vikao kazi vya Waziri wa Maliasili na Utalii kusikiliza changamoto za Watumishi na kuangalia namna ya kuzipatia ufumbuzi.

Please follow and like us:
Pin Share