Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kisarawe

Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani, Petro Magoti ametoa saa 24 kwa watu wanaodaiwa kukimbia na kuacha pikipiki wakiwa wanatorosha korosho kilo 600 kutoka Kisarawe wakielekea Kibiti.

Magoti ameonya kuwa ,yeyote atakayebainika akitorosha korosho kutoka wilaya hiyo, kwa kutumia chombo chochote cha moto, atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Akitoa taarifa ya tukio hilo lililotokea kata ya Marui,ambapo korosho hizo zilikuwa zikisafirishwa kwa njia za panya kwa usafiri wa pikipiki , oktoba 14,2024, Magoti alisema watu hao wajisalimishe kabla Jeshi la Polisi halijaanza kuwasaka.

“Kisarawe hatutaki mchezo wa ujanja ujanja. Ile shoo tunayosema, ndiyo tutaanza kuwapiga hawa,:'”

Nimetangaza motisha ya kiasi cha sh.200,000 kwa yeyote atakayekamata au kubaini mtu au watu wakitorosha korosho katika wilaya ya Kisarawe,” alisema Magoti.

Magoti alilipongeza Jeshi la Polisi, Idara ya Kilimo, na wananchi kwa kushirikiana kufanikisha kubaini watu hao.

“Yeyote atakayetorosha korosho, iwe kwa pikipiki, basi, au daladala, korosho hiyo itataifishwa, na hatua za kisheria zitachukuliwa. Huu ni uhujumu uchumi. Tumeshuhudia Rais Samia Suluhu Hassan akiwainua wakulima wadogo wa korosho,”

” Tumeona huko Mtwara korosho ikiuza hadi shilingi 4,150, lakini hapa Kisarawe wanatokea matapeli wanaowadanganya wakulima kuwa hakuna soko na wanachukua korosho kwa sh. 500 hadi 800,Haiwezekani!” alisisitiza Magoti.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Kisarawe aliongeza kuwa ,wakulima wanajitahidi kujiinua kimaisha kupitia kilimo cha korosho, hivyo wanahitaji kusaidiwa kuimarisha kipato chao, badala ya kudidimizwa kimaisha.

Please follow and like us:
Pin Share