Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa wananchi wote wenye sifa kuhakikisha wanashiriki katika uchaguzi muhimu wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024.

Rais Samia amesema kuwa uchaguzi huo utatoa mwelekeo wa Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025.

Akizungumza na wananchi wakati wa hitimisho la mbio za Mwenge kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza, leo Oktoba 14, 2024, Rais Samia alieleza kuwa Serikali za Mitaa ni mamlaka muhimu katika kubuni, kusimamia, na kutekeleza mipango ya kiuchumi na kijamii kwa maendeleo jumuishi ya wananchi.

“Nichukue fursa hii kuwasihi wananchi wote wenye sifa kuhakikisha wanashiriki kwenye uchaguzi huu muhimu. Ili tuweze kushiriki kama wagombea na wapiga kura, ni lazima kwanza tuwe tumejiandikisha,” alisema Rais Samia.

Rais Samia aliongeza kuwa zoezi la uandikishaji linaendelea hadi tarehe 20 Oktoba, 2024.

“Nina furaha kuwajulisha kuwa tayari nimejiandikisha katika orodha ya wapiga kura kwenye makazi yangu, kitongoji cha Sokoine, kijiji cha Chamwino Ikulu. Wananchi wote nawasihi twende kwenye maeneo yetu tukajiandikishe ili tuweze kushiriki uchaguzi wa tarehe 27 Novemba, 2024,” aliongeza Rais Samia.

Pia, Rais Samia aliendelea kueleza kuwa uchaguzi huo ni fursa kwa jamii kukuza demokrasia na maendeleo katika maeneo yetu, akinukuu msemo wa vijana, “Uchaguzi huu tusiuchukulie poa.”

“Napenda kuwakumbusha wananchi kutofautisha orodha ya wapiga kura inayotumika katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ambalo hutumika wakati wa Uchaguzi Mkuu,” alisisitiza Rais Samia.

Mwisho alimshukuru Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Kwa kufanya uzindizi wa wiki ya Vijana tarehe 11, Oktoba 2024

Wananchi mbalimbali waliojitokeza kuhitimisha Kilele cha Mbio za Mwenge ambazo kitaifa zimefanyika Jijini Mwanza katika Uwanja wa CCM Kirumba tarehe 14 Oktoba, 2024.

Please follow and like us:
Pin Share