Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mashindano ya mchezo wa kuogelea kwa wale wenye mahitaji maalumu yaendeshwa kwa mara pili jijini Dar es Salaam.

Mashindano hayo yalifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita siku ya jumamosi ya oktoba 12 mwaka huu katika bwawa la shule ya Shabaan Robert iliyoko Upanga, Dar es salaam.

Kwa msimu huo wa pili wa mashindano hayo ulijumuisha waogeleaji wenye changamoto mbalimbali ambao wakishindana kwa kuzingatia umri wao.

Katika hafla ya mashindano hayo mgeni rasmi alikuwa ni mwenyekiti wa Kamati ya Paralimpiki nchini Tuma Dandi .

Akizungumza katika hafla hiyo mwenyekiti huyo alieleza kuwa wanafarijika kuona watu wenye ulemavu wameitikia wito wa kushiriki katika michezo kwani michezo inatumika kama njia ya kuhamasisha mambo mbalimbali yakiwemo umoja na upendo.

“Watu wenye ulemavu wamekuwa na madhila mengi na hasa ukizingatia kuuishi ulemavu si kazi nyepesi. Tumefarijika kuona wadau wameanza kutuelewa nini kusudio letu la kuwapa nafasi ya kuonyesha walichonacho vijana hawa. Michezo tunaitumia kuhamasisha upendo pamoja ujumuishwaji katika mambo mbalimbali kwani hakuna aliyependa kuwa changamoto hiyo.”

Aidha mwenyekiti huyo aliongeza kwa neno la shukraaan kwenda kwa wadhamini waliosaidia kwa namna mbalimbali kufanikisha mashindano na kusema kuwa mashindano hayo yamefanyika yakiwa na lengo la kupata timu ya taifa ambayo itakwenda kushiriki mashindano ya paralimpiki ya dunia yatakayofanyika mwaka 2028 nchini Marekani.

“Nipende kutambua na kuthamini mchango wa wadhamini wote ambao wamesaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha mashindano haya licha ya changamoto zilizopo lakini mmeamua kujitoa kudhamini mashindano haya. Mashindano haya yanafanyika ikiwa kama ni maandalizi ya kuunda timu ya taifa ya mchezo wa kuogelea kwa watu wenye ulemavu kwaajili ya kushiriki mashindano ya paralimpiki mwaka 2028 nchini Marekani.”Alisema.

Kwa upande wa muwakilishi kutoka baraza la michezo la taifa, Afisa michezo Nicholas Mihayo naye alianza kwa kutoa rai kwa vyama vingine vya michezo kufuata mfano wa chama hicho cha kuongelea kwani walemavu wako wengi katika jamii zetu na wanahitaji pia ushirikishwaji katika michezo.

Mbali na hilo pia Afisa Mihayo aliongeza kwa kugusia juu ya mpango wa serikali katika kuboresha miundombinu ya michezo hususani mchezo wa kuogelea.

“Nimefurahi kuwepo hapa kuona waogeleaji hawa wenye mahitaji maalumu wakionyesha vipaji vyao katika michezo. Navielekeza vyama vingine vya michezo kufuata mfano wa chama hichi cha kuogelea kuwapa nafasi watu wenye ulemavu kushiriki katika michezo kwani vijana wenye mahitaji maalumu wako wengi katika jamii zetu na wanahitaji kuonesha walichonacho katika michezo”

“Serikali iko nyuma ya vyama vya michezo kuvisaidia kuhakikisha vinafanya vizuri na mchango huo unaenda sambamba na utengenezwaji wa viwanja vya kisasa vya michezo ambavyo vitakuwa katika uwanja wa Benjamin mkapa ambapo mojawapo pia ni bwawa kubwa la kuogelea la kisasa kukidhi vigezo vya kimataifa” Alisema.

Aidha kwa upande wa wadhamini ambao walishiriki katika kudhamini mashindano hayo ambapo miongoni mwake Hospitali ya tiba ambayo kupitia mkurugenzi mwendeshaji wake Arun Sharma ameelezea kwa namna walivyoguswa kudhamini mashindano hayo kwani wamebaini kuwa watu wenye mahitaji maalumu yanahitaji msaada mkubwa tofauti na wengine katika jamii hivyo wametumia fursa hiyo kuwa karibu zaidi na jamii kwani wanahusika na utuaji huduma za kijamii kwa asilimia zote.

“Sababu kubwa zaidi ya sisi kuwepo hapa hii leo ni kwakuwa tunatambua kuwa jamii ya watu hawa wenye mahitaji maalumu inahitaji msaada zaidi tofauti na jamii nyingine za kawaida . Sisi kwetu tumeona ni nafasi kwetu kuwasaidia watu hawa ikiwa sehemu mojawapo pia ya kujiweka karibu zaidi na jamii” Alisema.

Kwa nafasi nyingine pia kampuni ijushughulishayo na huduma za utoaji ya Blue dot nayo imeshiriki katika mashindano hayo ikiwa kama wadau waliodhamini kufanikisha mashindano hayo. Akizungumza mara baada ya hafla hiyo Afisa wa habari na mawasiliano kutoka kampuni ya Blue dot, Innocent Jonas ameeleza kuwa kama taasisi hiyo imekuwa ikijihusisha na huduma kwenda kwa jamii wameamua kuchangia kwa kiasi kuhakikisha wanawapa faraja vijana hao wenye mahitaji maalumu juu ya ushiriki wao katika michezo.

“Sisi kama kampuni tumeguswa kushiriki katika nafasi ya kudhamini mashindano haya kwakuwa sisi wenyewe tumekuwa tukishughulika na utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii hivyo kwa kulitambua hilo tumeamua kushiriki kufanikisha mashindano haya ili kuwapa faraja watu hawa wenye mahitaji maalumu katika upande wa michezo.” Alisema.

Wadhamini wengine ambao pia walishiriki kuwezesha tukio hilo ni pepsi, talliss club, pigec, flame na wengineo.

Please follow and like us:
Pin Share