Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

TAASISI ya Moyo ya (JKCI), imeanza kambi ya siku nne ya kupima na kutibu maradhi ya moyo kuanzia kesho kwa wakazi wa Mkoa wa Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge alisema wameandaa kambi hiyo kwa kushirikiana na Arusha Lutheran Medical Center (Selian ya Mjini).

Dk. Kisenge alisema pia wameshirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kuandaa kambi hiyo ambayo wanatarajia kuwafanyia uchunguzi watu wengi na kuwapa matibabu wale watakaobainika kuwa na matatizo ya moyo.

Alisema kambi hiyo itaendeshwa kuanzia leo Jumanne tarehe 15 mpaka 18 katika viwanja vya Arusha Lutheran Medica Center na kwamba watakaohudumiwa ni pamoja na mikoa jirani na Arusha.

Aliwaomba wananchi wa Arusha na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kupima afya zao kwani watakaogundulika kuwa na matatizo ya moyo watapatiwa matibabu na wengine kupewa rufaa kwenda Dar es Salaam kutibiwa JKCI.

Alisema kwenye kambi hiyo wataalamu wa lishe watakuwepo kutoa elimu kuhusu namna ya kula vyakula ili kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo.

“Watu wajitokeze watumie fursa hii kwasababu watakaobainika kuwa na matatizo ya moyo watapatiwa matibabu hapo hapo au kupewa rufaa kwenda JKCI Dar es Salaam,” alisema

Alisema jamii inapaswa kujenga utamaduni wa kupima afya ya moyo mara kwa mara kwani baadhi ya watu wamekuwa wakishi na maradhi hayo bila kujua lakini iwapo wangepima wangegundua na kupatiwa matibabu mapema.

Alisema wananchi wanapaswa pia kuzingatia ushauri wa wataalamu kuhusu lishe bora kwani wakizingatia lishe bora wataepuka maradhi mengi hasa yasiyo ya kuambukiza kama moyo.

“Wananchi wanapaswa kuzingatia lishe bora na kuwasikiliza wataalamu kuhusu ulaji unaofaa utakaowaepusha na maradhi mbalimbali yasiyo ya kuambukiza ambayo mengi yanatokana na ulaji usiofaa na wataalamu wa JKCI watakuwepo Arusha kuwapa elimu hiyo,” alisema Dk. Kisenge

Alisema JKCI imeendelea kujiimarisha kwa kuwa na vifaa tiba vya teknolojia ya kisasa na wataalamu bobezi wa moyo hali ambayo imepunguza utegemezi wa kupeleka wagonjwa wa moyo kwa matibabu nje ya nchi kwa zaidi ya asilimia 90.

Dk. Kisenge alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza kwenye taasisi hiyo ambayo sasa imekuwa kimbilio kwa mataifa mengi ya Afrika kutokana na kuwa na madaktari bingwa bobezi na vifaa vya kisasa kama vile vilivyoko nchi zilizoendelea.

Alisema baadhi ya mataifa ya Afrika yamekuwa yakiwaomba madaktari wa JKCI kwenda kutoa mafunzo ya utaalamu wa kibingwa wa matibabu ya moyo kwenye nchi zao na kuongeza kuwa hivi karibuni watalaamu wake walikuwa nchini Zambia kwa kazi kama hiyo.

Dk Kisenge alisema JKCI ilikuwa ikitoa matibabu kwenye maonyesho ya madini mkoani Geita kwa kushirikiana na hospitali ya kanda ya Chato.

Alisema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na hospitali zote nchini kuhakikisha wanatimiza ndoto za Rais Samia Suluhu Hassan kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii tiba.

“Kwenda Arusha ni mwendelezo wa kile tulichokuwa tukikifanya kwenye maonyesho ya madini tukishirikiana na hospitali ya kanda ya Chato,” alisema

Naye Profesa Mohamed Janabi ambaye ni Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alishukuru jitihada na ubunifu wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kwa kushirikiana na hospitali za mkoa huo kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha utalii tiba.

Please follow and like us:
Pin Share