Na Gerald Malekela, JamhuriMedia, Iringa

Katika juhudi za kukuza uchumi, Tanzania imekuwa ikitarajia sera na mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuongeza pato la taifa.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni utoaji wa misamaha au unafuu wa kodi na juhudi za kuongeza ukusanyaji wa rasilimali za ndani (DRM).

Ukusanyaji mzuri wa kodi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha uchumi unakua kwa kasi na unawezesha maendeleo endelevu.

Ndiyo maana mara zote serikali imekuwa ikitekeleza sera na sheria za kodi na kuweka misamaha au unafuu wa kikodi kwa lengo la kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Vivutio hivyo vinajumuisha punguzo la kodi, misamaha ya kodi na taratibu rahisi za kikodi zinazowahamasisha wawekezaji kuwekeza katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, utalii, viwanda na nishati.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya mwaka 2024, kuna idadi ya vivutio vya kodi (msamaha na makato).
Kwa mfano, sekta ya kilimo, serikali imetoa misamaha ya kodi katika vifaa vya kilimo na pembejeo kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kupunguza gharama za uzalishaji.

Hatua hiyo imechangia kuongeza uzalishaji wa chakula na mazao ya biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia pato linalotokana na sekta ya kilimo.

Katika sheria hiyo imeonyesha namna mwekezaji wa kampuni zinazopata hasara kwa miaka mitatu mfululizo isipokuwa zinazofanya shughuli za kilimo, afya na elimu ni asilimia 0.5 ya mauzo ya mwaka kwa kampuni za ndani huku zile za kigeni ni asilimia 0.

Sheria hiyo inatoa fursa kwa kampuni ya nje kushindwa kuchangia hata kiasi kidogo cha pato la taifa kwa miaka mitatu mfululizo endapo haitafikia malengo yake huku ikimbana mwekezaji wa ndani.

Vilevile, sekta ya viwanda imefaidika na sera hizo na wawekezaji wamehamasishwa kuwekeza katika viwanda vya uzalishaji wa bidhaa za ndani.

Profesa wa Uchumi na Jiografia wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abel Kinyondo (kushoto), akitoa mafunzo ya masuala ya kodi na uwajibikaji kwa waandishi wa habari jijini Dodoma hivi karibuni. Mafunzo hayo yaliandaliwa na Shirika la Policy Forum.

Hatua hiyo imewezesha kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje, jambo linalosaidia kuimarisha mtiririko mzuri wa biashara, hivyo kuongeza pato la taifa.

Pia sheria hiyo inaipa unafuu mkubwa kampuni mpya ya nje iliyoanzishwa kwa ajili ya kutengeneza mitambo na mashine ya kuunganisha magari, matrekta na boti za uvuvi na injini za nje ya boti, yenye makubaliano ya kiutendaji na serikali kwa kipindi cha miaka mitano ya mwanzo tangu kuanza uzalishaji huku zikiwa hazilipi kodi wakati za ndani zinalipa asilimia 10.

Kupitia sheria hii, serikali imekuwa ikipoteza mapato mengi kutoka kwa wawekezaji wa nje kupitia sheria hii.
Pia kampuni mpya za viwanda vya dawa za binadamu na viwanda vinavyotengeneza bidhaa za ngozi zenye mkataba wa makubaliano na serikali, zitapata punguzo la kodi ya mapato kwa miaka mitano ya mwanzo tangu kuanza uzalishaji huku zile za kigeni zitalipa asilimia 0 na zile za ndani zitalipa asilimia tano. Je, ni kiasi gani cha fedha serikali inapoteza na kwa nini isingekuwa hata asilimia mbili tu kwa mwekezaji wa nje?

Juhudi za ukusanyaji wa rasilimali za ndani, kama vile kodi na ada zina mchango mkubwa katika kuongeza pato la taifa.

Ukusanyaji wa mapato ya kodi unasaidia serikali kugharamia huduma muhimu kama vile elimu, afya, miundombinu na miradi mingine ya maendeleo.

Pamoja na mambo mengine, Tanzania imepiga hatua kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa kodi kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kujikita kuongeza ufanisi na kupunguza mianya ya ukwepaji kodi.

Kwa mfano, matumizi ya teknolojia ya kisasa ya ukusanyaji wa kodi, kama vile mashine za kutolea risiti kwa njia ya kielektroniki (EFDs) yameongeza uwazi na kupunguza ukwepaji kodi.

Hii imeiwezesha serikali kuongeza mapato yake ya ndani yanayotumika moja kwa moja katika miradi ya maendeleo ya kitaifa.

Makusanyo ya TRA

Katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha wa 2023/2024, TRA imefanikiwa kukusanya Sh trilioni 6.63, sawa na ufanisi wa asilimia 95.17 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 6.97.

Mamlaka hiyo ilisema makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 11.68 ikilinganishwa na makusanyo ya Sh trilioni 5.94 ya kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Taarifa hiyo inasema Machi 2024, TRA imefanikiwa kukusanya Sh trilioni 2.49, sawa na ufanisi wa asilimia 97.05 katika lengo la kukusanya kiasi cha Sh trilioni 2.56.

Makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 6.91 ukilinganisha na kiasi cha Sh trilioni 2.32 kilichokusanywa mwezi kama huo katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Hata hivyo, TRA imekuwa ikisisitiza uwajibikaji wa wananchi kulipa kodi na kujenga uelewa kuhusu umuhimu wa kodi katika maendeleo ya taifa.

Kupitia kampeni za kuhamasisha ulipaji kodi, wananchi wengi wanaelewa wajibu wao wa kuchangia mapato ya serikali.
Kimsingi, kuna uhusiano mkubwa wa msamaha, unafuu wa kodi na ukusanyaji wa rasilimali za ndani.

Misamaha na unafuu wa kodi unachochea uwekezaji na uzalishaji unaongeza ajira na uzalishaji wa bidhaa na huduma, hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi.

Kwa upande mwingine, ukusanyaji wa rasilimali za ndani unahakikisha serikali inapata mapato ya kutosha kugharamia miradi ya maendeleo na huduma za kijamii.

Licha ya jitihada hizo lakini hivi karibuni serikali imekiri kushuka kwa makusanyo ya kodi. Kupitia taarifa iliyochapwa na Jarida la Kimataifa la DW la Aprili 27, mwaka huu limeonyesha makusanyo hayo yalivyoshuka.

Taarifa hiyo inasema ukusanyaji wa mapato yatokanayo na kodi hapa nchini ni chini ya asilimia 12 ya pato la taifa, hali inayochochewa na mwamko mdogo wa ulipaji kodi wa Watanzania wakati nchi nyingine za Afrika zikiwa na asilimia ya juu ya makusanyo hayo.

Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, anasema ukusanyaji mdogo wa kodi unachangia hali mbaya ya uchumi na akataka mamlaka husika kufanya jitihada za kukusanya angalau kwa asilimia 15 ya pato la taifa.

Kiwango hicho ni chini ya wastani wa asilimia 15.6 ya zaidi ya pato la taifa kwa nchi za Afrika. Akasisitiza kufanyika kwa maboresho ya sheria, sera na viwango vya kodi, kuendelea kuimarisha vituo jumuishi vya huduma za uwekezaji na kupunguza viwango vya ushuru wa forodha.

Waandishi wa habari wakijadiliana jambo wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Policy Forum kuhusu masuala ya kodi na uwajibikaji jijini Dodoma hivi karibuni.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, anasema changamoto kubwa katika sekta hiyo ni ulipaji wa kodi kwa hiyari na utoaji wa risiti, huku wafanyabiashara wakiwa vinara, wakiwaongoza wanunuzi kukwepa kodi.

Mwaka 2023 Shirika la Sikika nchini Tanzania lilitoa ripoti yake kuhusu sababu za wafanyabiashara kutokulipa kodi na utafiti huo uliainisha mambo kadhaa, ikiwamo utitiri wa kodi, mlolongo mrefu wa mchakato wa ulipaji kodi na wakusanyaji wa kodi kutumia nguvu wakati wa kukusanya kodi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, anasema serikali imeendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji.

Pia kumekuwapo na jitiahada zinazofanywa na serikali pamoja na wadau mbalimbali kama Shirika la Policy Forum kutoa elimu kwa wanahabari na jamii kuhusu masula ya umuhimu wa kulipa kodi na matumizi sahihi ya kodi katika maendeleo ya taifa.

Kwa sababu ukuaji wa pato la taifa unaochangiwa na mikakati hii pia unatoa nafasi kwa serikali kupanua wigo wa unafuu wa kodi na kuboresha sera za kikodi ili kuvutia wawekezaji zaidi. Hii inasababisha mzunguko endelevu wa kiuchumi.

Akizungumza jijini Dodoma hivi karibuni katika mafunzo kwa wanahabari yaliyoandaliwa na Policy Forum, Profesa wa Uchumi na Jiografia wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Abel Kinyondo, anasema ukuaji wa uchumi endelevu na ongezeko la pato la taifa litokanalo na kodi hapa nchini unawezekana.

Profesa huyo wa DUCE anasema ukuaji huo unawezekana ikiwa jitihada hizo zitaimarishwa, kusimamiwa na kukawa na uwajibikaji na uadilifu kwa kila sekta na kupitia upya sheria za kodi tulizonazo kwa wawekezaji wa ndani na nje hususan misamaha na unafuu wa kodi.

Please follow and like us:
Pin Share