Na Mwandishi Wetu

Kada wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) anayeshitakiwa kwa kosa ka kusambaza taarifa za uongo kwenye mtandao wa X kuwa ameshambuliwa na watu wasiojulikana mjini Iringa, Vitus Nkuna (29) amefungiwa leseni ya udereva kwa miezi sita.

Akizungumza na wanahabari leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi amesema adhabu hiyo inayomtaka pia kulipa faini imeanza Oktoba 7, mwaka huu.

Amesema Nkuna amepewa adhabu hiyo kwa kosa la kuendesha gari akiwa amelewa na kusababisha ajali akiwa anaendesha gari yenye namba za usajili T797 DYC aina ya Volkswagen na kugonga gari yenye namba T975 EDC aina ya Toyota Probox katika tukio lililotokea Septemba 30, 2024.

“Tulimkamata Nkuna kwa makosa mawili, moja ni kusababisha ajali ambalo hukumu yake ndio hiyo ya kufunguwa leseni na kosa la pili ambalo shauri lake linaendelea mahakamani ni kutoa taarifa hizo za uongo katika mtandao wa X,” amesema.

Mbali na Nkuna aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo wa Kanda ya Nyasa (Bavicha) Bukumbi aliwataja wengine waliopata adhabu ya kufungiwa leseni kwa miezi sita kuwa ni pamoja na:

“Musa Omary (40) mkazi wa Dodoma aliyefungiwa leseni toka Septemba 3, mwaka huu hadi shauri lake litakapokwisha mahakamani kwa kosa la kumgonga mtembea kwa miguu Martine Mgaya katika eneo la Ifunda akiwa anaendesha gari lenye namba za usajili DFPA 9917 aina ya Toyota Land Cruiser na kumsababishia kifo.

Mwingine ni Cleophas Mahaki (37) aliyefungiwa leseni toka Septemba 10, mwaka huu kwa kosa la kulipita gari iliyokuwa mbele yake kwenye kona kali eneo la Mlima Kitonga bila kuchukua tahadhari akiwa anaendesha gari yenye namba T710 DPS basi aina ya Yutong mali ya kampuni ya Mbeya City.

Wakati huo huo SACP Bukumbi alisema jeshi lake linamshikilia Olivo King’unza mfanyabiashara mkazi wa Mafinga kwa kujifanya mtumishi wa Jeshi la Kujenga Taifa aliyemtaka muhudumu wa nyumba ya kulala wageni ya Nyembeche ya mjini Kilolo ampatie Sh 500,000 ili amuingize jeshini.

Katika tukio lingine jeshi hilo limemkamata Benny Malangalila (22) na watuhumiwa wengine wanne wakiwa na nyara za serikali ambazo ni nyama ya swala vipande 20, nyama ya digidigi vipande 12, na nyama ya nungunungu vipande 10.

Zingine ni mkia na miguu minne ya Tandala, na mnyama pori aina ya kakakuona akiwa hai ndani ya boksi wakitafuta mteja kwa ajili ya kumuuza.

Aidha katika doria na misako yao inayoendelea alisema wamekamata watuhumiwa 46 kwa makosa ya wizi wa mali mbalimbali zikiwemo pikipiki 23, runinga tisa, simu nne, madumu 10 yakiwa na mafuta ya dizeli, na redio tatu.
“Katika kupambana na matumizi na biashara ya dawa za kulevya, tumewakamata watuhumiwa saba wakiwa na jumla ya kete 95 pamoja na vifurushi 30 vya dawa za kulevya aina ya bangi.

Please follow and like us:
Pin Share