Mpendwa msomaji nakutakia heri ya mwaka mpya 2018. Mungu alipo hakuna cha kuharibika. Nikiri kuwa katika kuumwa nimepata fursa ya kufahamu Watanzania wanavyofuatilia kazi ya mikono yangu na hasa hili suala la muhogo.
Nimegundua kuwa Watanzania wengi wana nia ya kujiondoa katika lindi la umaskini. Sitanii, kwanza niwie radhi msomaji wiki iliyopita, makala hii ilikuwa na makosa ya hijai (spelling mistake) mengi.
Yalitokea makosa ya kiutendaji, ikachapishwa makala ambayo haikuhaririwa kabisa hali iliyozaa kosa hilo.
Nilitaka kurudia makala yote, ila baada ya kushauriwa na watu kadhaa, nimeona niombe radhi kwa njia hii niendelee na mada mpya.
Baada ya radhi hiyo, naomba tusonge mbele. Nashukuru baada ya makala ya wiki iliyopita nimeanza kupata mrejesho mzuri.
Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba amepata ushauri kutoka kwa wanasiasa wastaafu na waliopo madarakani, sasa ameanza kuunga mkono wazo la kilimo cha muhogo.
Ingawa hajarejea kwangu, ila nimesikia mipango aliyonayo ya kutaka kuimarisha kilimo cha muhogo.
Nimezungumza na mmoja wa mawaziri wastaafu na mwingine aliyeko madarakani, ambao wote wameniambia wamezungumza na Dk. Tizeba na kumwambia awasaidie wakulima wa Tanzania katika kilimo cha muhogo.
Lakini nimefarijika zaidi kutokana na simu ya Naibu Waziri wa Elimu, na Mkuu wa Mkoa (mstaafu), Mwantumu Mahiza.
Sitanii, mama huyu pia amekuwa mkuu wa mikoa ikiwamo Tanga na Pwani. Mazungumzo ya zaidi ya nusu saa kwenye simu, yamenipa faraja kubwa.
Amenipongeza kwa kuandika makala za muhogo. Amenijulisha kuwa sasa analima muhogo huko Tanga. Ameniambia kwa uchache kwamba analima ekari 20 za muhogo kila mwaka.
Mama Mwantumu ameniambia hivi: “ekari moja unapanda miche 4,000. Mihogo ikikomaa kati ya miezi sita au tisa, ninauza kila mti mmoja Sh 1,000. Kwa mantiki hiyo, kila ekari moja ninapata Sh 4,000,000.”
Maneno hayo yamenipa moyo mkuu. Mwaka huu na mimi naanza kilimo cha muhogo. Naomba kuwashirikisha Watanzania bila kutaja watu niliozungumza nao katika wiki hii iliyoisha. Wengi wamenipa ushawishi wa aina yake.
Nimeambiwa kuwa Tanzania kwa mwaka inatumia wanga wastani wa tani 40,000. Nchi yetu inazalisha tani 19,000 hivyo tani 21,000 zinaagizwa kutoka nje ya nchi.
Wanga unatumiwa katika viwanda vya bia, soda na nguo. Nchi yetu, mahitaji ya wanga yataongezeka kadri tunavyozidi kuwekeza katika viwanda.
Si hilo tu, nchi kama Nigeria zimeanza kutumia unga wa mihogo kulisha mifugo badala ya mahindi.
Unga wa mihogo unatumika kutengeneza biskuti, mikate, keki na vyakula vingine vingi. Huu ni mwaka mpya. Leo ni siku ya pili tangu tumeingia mwaka 2018.
Swali kubwa naomba ujiulize. Je, umepanga kufanya nini mwaka huu katika harakati za kuondoa umaskini katika familia yako?
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga mwezi uliopita ametembela China.
Katika ziara hiyo, Balozi Mahiga amekutana na wawakilishi wa kampuni ya Shandong Taianguiyu Food Co. Ltd na wakazungumzia nia ya kampuni hiyo kujenga kiwanda cha kutengeneza vyakula vya aina mbalimbali (noodles) kwa kutumia muhogo kwa ajili ya soko la China.
Kampuni hiyo imeeleza kwamba mwezi Machi, mwaka huu itatuma timu ya kufanya maandalizi ya uwekezaji nchini Tanzania.
Wameeleza kwamba kiwanda kitakapoanza kazi kitahitaji kununua muhogo tani 3,000 kwa siku kwa ajili ya uzalishaji.
Balozi Mahiga ameikaribisha kampuni hiyo kuja Tanzania na pia ameitaka ilete nchini teknolojia ya kuongeza tija (productivity) katika kilimo cha muhogo, kuwapa wakulima fursa ya kuzalisha kwa wingi na kuuza muhogo kwa kampuni hiyo.
Sitanii, hii ni fursa. Watanzania tujiandae kusimamia uchumi wa viwanda kupitia kilimo cha muhogo.
Nimeambiwa kuwa mkoa wa Pwani kimepata kuwapo kiwanda cha kuchakata muhogo, lakini kimekosa malighafi hadi kikafungwa.
Watanzania tujiandae, hakuna mjomba wala shangazi, `vyuma vilivyokaza’ sisi ndio wa kuvilainisha.
Heri ya Mwaka Mpya 2018.