Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga

Mkuu wa Wqilaya ya Handeni Mkoani Tanga Albert Msando amewahakikishia wananchi wanaoishi Tarafa ya Ngorongoro na wanataka kuhamia katika kijiji cha Msomera kutokuwa na hofu yoyote kuhusiana na maisha ndani ya kijiji hicho kwani ni salama na Serikali imekuwa ikitatua kila aina ya changamoto inayojitokeza ili wananchi hao waweze kuishi kwa umoja,amani, ushirikiano na utulivu.

Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho mwishoni mwa wiki Wakili Msando amesema kuwa tangu zoezi hilo kuanza mwezi Juni mwaka 2022 mpaka Septemba mwaka 2024 ameshapokea zaidi ya wananchi 9,976 na mifugo 40,397 jambo ambalo linaonesha wazi kwamba kadri wananchi wanavyoelimishwa wako tayari kuhama.

DC Msando amewaambia wanahabari hao kuwa Serikali ya wilaya ipo tayari kupokea makundi mbalimbali yanayotaka kufika katika kijiji hicho ikiwemo waandishi wa habari, wanaharakati na asasi zisizo za kiserikali kutoka ndani na nje ya nchi na kufanya kazi zao kwa uwazi ili waone kazi kubwa iliyofanywa na serikali.

“Tunataka kukifanya kijiji cha Msomera kuwa cha mfano ambapo dunia itakuja kujifunza namna haki za binadamu zionavyoheshimiwa na tunayafanya haya ili kuwaondoa kwa hiari wananchi wetu wanaoishi katika Tarafa ya Ngorongoro katika dimbwi la umaskini na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ndani ya hifadhi ikiwa ni pamoja na kulinda maisha yao,” alisema Msando.

Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza kuwa hivi sasa dunia inasisitiza kuhakikisha malengo ya milenia yanatimizwa ambapo kufikia mwaka 2030 kila mwananchi aweze kupata huduma zote muhimu za kijamii na ndicho ambacho serikali ya Tanzania inakitekeleza kwa kuwahamisha wananchi kwa hiyari kutoka Tarafa ya Ngorongoro kwenda Msomera na Maeneo mengine ambayo wananchi hao watakayoyachagua.

Waandishi hao wa habari za uhifadhi wamempongeaa mkuu huyo wa Wilaya kutokana na kazi kubwa aliyoisimamia katika kijiji hicho na kufanya maisha ya wananchi kubadilika na kuwa yenye tija ambapo wananchi hao wameweza kujengewa uwezo na kuanza kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Katika ziara hiyo waandishi hao walitembelea katika Tarafa ya Ngorongoro na kujionea hali halisi ya mazingira katika eneo hilo pamoja na ongezeko kubwa la watu na mifugo ambapo walipofika katika kijiji cha Msomera wamejionea mabadiliko makubwa ya kiuchumi ya wananchi waliohama kwa hiari.

Please follow and like us:
Pin Share