Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Rais wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jaji Mstaafu Bernard Luanda, amewashauri waandishi wa habari, kuandika habari zisizo na mlengo mbaya na badala yake kuandika habari zinazoelimisha wananchi hasa kwa kipindi hiki tunachoelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali ya Mtaa na Uchaguzi Mkuu 2025.

Hayo ameyabainisha leo Oktoba 4, 2024 wakati alipotembelea ofisi za Kampuni Jamhuri Media Limited jijini Dar es Salaam wakati akitambulishwa kwenye vyombo vya habari na Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura baada ya kuchaguliwa hivi karibuni.

Rais wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jaji Mstaafu Bernard Luanda, akizungumza katika ofisi za gazeti la Jamhuri Media jiji Dar es Salaam leo Oktoba 4, 2024

Jaji Luanda amesema kuwa ni vyema kuandika habari zinazoelisha jamii ambazo zitasaidia kutoa uamuzi sahihi kwa wananchi wa nani anayefaa kuwaongoza na kufahamu kuwa nchi inaongozwa kwa utawala bora.

“Taaluma hii ni nyeti sana ya uandishi wa habari na ndio maana utakuta viongozi wengi hasa wa kisiasa wanashida, wanashida kwamba hawapendi yale ambayo wanataka yasitoke lakini wananchi wanataka yale ambayo hayatoki ndio wanayapenda ili wajue kilicho huko ndani.

“Hivyo nitoe tahadhari kwamba muwe waangalifu sana na kuchukua tahadhari zote ili msipate madhara makubwa, ingawa madhara mtayapata lakini yasiwe makubwa.

“Cha msingi fanyeni kazi, elimisheni wananchi ili wapate mambo ambayo yatawasaidia baadae kutoa uamuzi katika chaguzi kwani itakuwa nzuri zaidi kama watakuwa wamepata taarifa nzuri na wakafanya uchaguzi ambao utawasaidia kujua ni nani anafaa kwani itasaidia kuchagua kiongozi bora na kufahamu nchi yetu inaongozwa kwa utawala bora” amesema jaj Luanda.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jamhuri Media Limited, Deodatus Balile, akizungumza wakati wa kikao hicho.

Ameongeza kuwa katika kipidi cha chaguzi wanasiasa wanakuwa na kaupendeleo fulani na wanapenda kusifiwa sasa ni vyema waandishi wa habari mkawa makini sana na si kuwekwa mfukoni bali ni vyema mkawa wawazi kwenye hapana iwe hapana na kwenye ukweli pawe ukweli na kwa kufanya hivyo itasaidia.

“Kuna gazeti moja nilikuwa nalipenda sana (sitaki kulitaja jina lake) lakii siku hizi si kama zamani kwani halipo sawa kama mwanzo, lilikuwa linaandika ukweli, linazungumza ukweli na habari wanazotoa zilikuwa zinagonga mahala pazuri na wananchi wanapata elimu” amesema jaji Luanda.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jamhuri Media Limited, Deodatus Balile, amempongeza Katibu Mtendaji wa MCT, Sungura kutokana na kufanya mabadiliko makubwa katika utoaji wa tuzo zilizopita pia ushirikishwaji katika upatikanaji wa rais MCT ambapo zamani ilikuwa ni kuona kwenye matangazo.

Mhariri Mkuu wa Gazeti la Jamhuri Joseph Beda

“Hii ni hatua kubwa kwa MCT na tunaamini kuwa haya mabadiliko yataedelea kutokea kwani hivi sasa Jamhuri Media ina miaka 13 tagu ilipoanza rasmi 2011 ambapo tumejaribu kwenda mkondo wa uchunguzi na tunaendesha gazeti la wiki la uchunguzi.

“Katika kufanya hivyo tumeona ni eneo ambalo linapungukiwa sana katika nchi yetu na tumekuwa na shida moja ya msingi ambayo ni ‘resources’, vyanzo vya mapato na sehemu nyingi duniani magazeti yamepata shida ya matangazo kupungua” amesema Balile.

Balile amesema kuwa kutokana na teknolojia kukua duniani hivi sasa watu wengi wamekuwa na hamu ya kwenda online kuliko kusoma magazeti lakini hayo ni maadiliko ambayo hayatuogopeshi sana lakini yanatia woga kwa watu ambao hawajiandaa kwa maana wanawaza magazeti yanakwisha, magazeti yanakufa.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura akizungumza kuhusiana na ziara hiyo katika ofisi za gazeti la Jamhuri.

Balile amesema kuwa kutokana na kukua kwa teknolojia watu walijua hata kuandika barua ni mwisho lakini mpaka leo watu bado wanaandika barua na magazeti yanaendelea kukua mpaka sasa hatua teknolojia zaidi.

“Sasa imekuja hii ya online lakini umuhimu wa magazeti hauondoki bado upo pale pale, kinachobadilika ni njia ya magazeti inavyowafikia wasomaji, nasi tunapaswa kuhama na kwenda online na lakini ni vizuri online ikaenda ikiwa na ‘Quality content’ na pia hakuna kilichobadilika kwenye uandishi wa habari, kilichobadilika ni kitu kimoja tu ni suala la muda.

Rais wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jaji Mstaafu Bernard Luanda (kushoto) akiangalia tuzo iliyopewa Kampuni ya Jamhuri Media Limited ya kuwa miongoni mwa Kampuni Bora ya Vyombo vya Habari inayowasilisha michango ya wafanyakazi ya NSSF kila mwezi na kwa wakati bila kuchelewesha.

‘Zamani ilikuwa ikitokea ajali pale Senkeke waandish wanaandika ajali kubwa…. siku inayofuata majina ya abiria waliofariki watajwa,siku inayofuata majina ya majeruhi yatajwa, siku inayofuata majeruhi waanza kutoka hospitalini, siku inayofuata daktari atangaza….yaani utakuta wiki nzima watu wanafuatilia kwenye magazeti.

“Lakini siku hizi mtu ana simu yake ya Smart phone anatoa taarifa nyumbani jinsi ajali ilivyotokea na jinsi alivyoumia na kwa teknoljia hii mtu huyu hawezi ununua gazeti la siku inayofuata.

“Hivyo tunahitaji kumpa taarifa kwenye ‘online’ ya kina ambayo itamfanya afanye uamuzi wa nyongeza wa kuipata taarifa hiyo kwa kina kwenye mtandao hivyo sisi waandishi tunapaswa kuziba hilo obwe la habari ambalo lipo kwenye mtandao wa kijamii hivi kwani ni jangwa la habari kutokana na kila mtu ambaye si mwandishi wa habari kuweka taarifa mtandaoni.

“Sasa tusibe hilo kwa kuweka taarifa za kina ‘quality content’ shida inayokuja ni kwamba tutatengenezaje pesa online kutokana na kutolipiwa hivyo tunatakiwa sasa kutengeneza njia nyingie itakayotusaidia kuzalisha kipato.

“Ili tujue ni jukumu la msingi na si biashara bali ni taaluma hivyo tufanye kazi ya kuelimisha,kuburudisha na kuhabarisha kwani hakuna kifungu kinachosema na kutengeneza faida hivyo cha msing ni kutafuta fedha katika vyanzo vingine” amesema.

Hata hivyo ametumia nafasi hiyo kumpongeza Jaji Luanda kwa kuchaguliwa kushika nafasi ya Rais wa MCT.

Naye Katibu Mtendaji wa MCT, Sungura amesema kuwa nia ya kufika katika ofisi hizo ni kumtambulisha rais huyo ambaye amerithi mikoba ya Jaji Juxon Mlay aliyefariki dunia mwaka akiwa nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu kutokana na changamoto za kiafya zilizokuwa zikimkabili.

Baadhi ya wafanyakazi wa Jamhuri Media wakiwa katika picha ya pamoja Rais wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jaji Mstaafu Bernard Luanda,
Please follow and like us:
Pin Share