Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Serikali imewataka Wataalam wa Maabara za binadamu nchini kuilinda taaluma yao kwa kuwa ina mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za afya kwa jamii.

Naibu Waziri Mkuu wa Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema hayo leo Oktoba 2, 2024 Jijini Dodoma wakati akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Kongamano la 37 la Kisayansi la Wataalamu wa Maabara za Afya nchini na Kongamano la 23 la Kisayansi la HUOQAS na Mkutano Mkuu wa Mwaka.

“ Wito wangu kwenu ioneeni wivu, muipende na kuithamini taaluma yenu, msikae pembeni mnapoona kuna changamoto semeni bila kuogopa. Wataalamu wa Maabara bila ninyi tiba haiwezi kufanyika na mfanye kila mtu awaheshimu,” amesema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko amesisitiza “ Nataka niwaambie mnapofanya kazi hii mnawahudumia Watanzania tufanye kwa upendo na tuwape majibu sahihi ili kuisaidia Serikali yetu kuwa mhudumu wa kweli wa wananchi.”

Aidha, Dkt. Biteko ameelekeza waajiri nchini kuruhusu watumishi wao wa kada ya maabara kushiriki katika makongamano ya kitaaluma huku akiwataka washiriki kujifunza kupitia mada zitakazowasilishwa na baadaye kuwashirikisha wataalam wenzao ambao hawakuhudhuria.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya itafanyia kazi changamoto zote zilizowasiliahwa na MeLSET.

“ Changamoto zote nimezichukua na naitaka Wizara kuchukua hotuba ya MeLSAT na kuzifanyia kazi changamoto zote zilizowasilishwa katika mkutano ili mwaka ujao changamoto zisiwe hizi tuwe na masuala mengine ya kuzungumza,” ameeleza Dkt. Biteko.

Naye, Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa Serikali imefanya maboresho makubwa kwenye sekta ya afya na hiyo inaonesha hatua kubwa imepigwa huku akitaja shilingi trilioni 1.2 zilizotumika kuboresha maabara za afya nchini.

Ametaja eneo lingine lililoboreshwa katika sekta hiyo ni vitendea kazi vya kiuchunguzi kwa uwepo wa vifaa vya kisasa zikiwemo mashine 13 za MRI Digital xray 346, ulta sound 476 na ufundishaji wa ubingwa bobezi.

“ Maboresho hayo yamegusa pia Mfuko wa ufadhili wa Rais Samia ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu pekee umeshagharamia kiasi shilingi bilioni 9 ili kusomesha wataalamu wa sekta ya afya hapa nchini. Tumetanua wigo wa utalii wa afya kupitia uwekezaji huu uliofanywa na Mhe. Rais Samia.” Amesisitiza Mhe. Mhagama.

Kaimu Mganda Mkuu wa Serikali, Dkt. Saitore Laizer amesema kuwa Wizara ya Afya imekuwa mstari wa mbele kukuza vyama mbalimbali vya kitaaluma ili viweze kusaidia kuishauri Serikali katika masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha sekta ya afya nchini.

Amebainisha kuwa baada ya Serikali kuwekeza katika vifaa tiba na miundombinu pamoja na watumishi suala kubwa ni kuhakikisha kuna ubora wa huduma za afya na kuwa hicho ni kipaumbele ili mambo yote yaliyofanyika yaweze kuwa na tija.

“ Suala la usugu wa vimelea vinaweza kuhama kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kama yalivyo magonjwa na ikifika huko maana yake tunaweza kupoteza maisha na gharama kubwa, “amesema.

Kwa upande wake Rais wa Chama Cha Wataalam wa Maabara za Afya Tanzania (MeLSAT), Bw. Yahya Mnung’a amesema kuwa lengo la Kongamano hilo ni kuwakutanisha wataalam na kutatua changamoto za kitaaluma katika maabara za binaadamu pamoja na uwepo wa maonesho ya vifaa vinavyotumika katika maabara za binadamu.

Ameongeza kuwa MeLSAT inaendelea kuimarisha ushirikiano na vyama vya kitaaluma nchini pamoja na nje ya nchi na kuwa Tanzania.

“ Maabara ya Afya ya Jamii ya Tanzania imekuwa ikifanya kazi nzuri na maabara yetu ni kati ya Maabara tatu bora barani Afrika. Tunaiomba Serikali iridhie ombi letu la kupandisha hadhi maabara hii ili kuwa Taasisi kwa kuwa inafanyakazi kubwa ndani na nje ya nchi,” amesema Bw. Mnung’a.

Ameongeza kuwa wataalamu hao wataendelea kutoa huduma kwa Watanzania licha ya uwepo wao kwa idadi ndogo.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Wataalamu wa Maabara za Afya Afrika (FeLPA), Bw. Mulate Mubanga amesema kuwa idadi kubwa ya watu hupata madhara kwa kutumia dawa bila kufanya vipomo vya maabara na kuwa ni vyema Serikali barani Afrika pamoja na wadau wa sekta hiyo kupatia ufumbuzi changamoto hiyo.

Please follow and like us:
Pin Share