Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Sumbawanga

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amezitaka Serikali za Vijiji kuweka ajenda ya uhifadhi wa mazingira na kudhibiti moto iwe za kudumu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadae.

Ameyasema hayo leo Oktoba 2, 2024 alipokuwa akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mponda, Wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa.

“Utunzani mazingira ni pamoja na kupanda miti, hivyo ni lazima tupande miti na tunaposafisha mashamba tuwe makini na matumizi ya moto” amesisitiza.

Aidha, ameendelea kuhamasisha wananchi kuwa na mizinga ya nyuki ili kupata asali itakayowasaidia kujiinua kiuchumi.

Katika hatua nyingine Chana amewaasa wananchi kuacha kuingiza mifugo hifadhini ili kuepukana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu.

Naye, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii (anayeshughulikia Maliasili) Kamishna Benedict Wakulyamba amewapongeza wananchi wa Kijiji hicho kwa kulinda Shamba la Miti Mbizi na kuwahimiza kuendelea kulinda misitu.

Waziri Chana yuko Mkoani Rukwa kwa ziara ya kikazi ya kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Please follow and like us:
Pin Share