*Mkoa waweka alama kujibu kwa vitendo katika sekta ya viwanda

*Kati ya viwanda 1,535, viwanda 131 vimejengwa kipindi cha Rais Dk Samia

Na Mwamvua Mwinyi, JakhuriMedia, Pwani

AJENDA ya kuleta Mapinduzi kwenye sekta ya Viwanda nchini, inazidi kushika kasi ambapo mkoa wa Pwani umejipambanua kuwa kinara kutekeleza ajenda hii kwa kuwa na viwanda 1,535 mwaka 2024 ,kutoka viwanda 396 mwaka 2016.

Hatua hii inaacha alama katika kuinua sekta ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji mkoani humo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025, inayolenga kuifanya nchi kuwa na uchumi imara unaotegemea viwanda.

Katika juhudi za kuendeleza sekta hii mkoani, huwezi kusahau mchango wa Mhandisi Evarist Ndikilo, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, ambaye aliweka msingi thabiti kwa kuongeza viwanda hadi kufikia 1,236 kabla ya kumkabidhi kijiti Alhaj Abubakar Kunenge Mei 20,2021.

Kunenge aliendelea kuvutia wawekezaji na kuhakikisha kuwa Pwani unasonga mbele zaidi na sasa kufikia viwanda 1,535 .

Kunenge anasema ,mafanikio hayo katika sekta ya Viwanda yamechangiwa pia na Royal Tour na uhamasishaji wa Serikali ya awamu ya sita, ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameweka mazingira bora ya uwekezaji nchini.

Mkuu huyo wa mkoa anajinasibu kuwa pamoja na ongezeko la viwanda pia kuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kongani 26 na maeneo mengine yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda hekta 24,240 .

“Tunajivunia kuufungua Mkoa wa Pwani kwa ujenzi wa viwanda ,tuna kongani tatu kubwa na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kongani 26 ,Tuna kila sababu ya kuishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuvutia wawekezaji na kuboresha mazingira wezeshi hatua kwa hatua ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili,”

Hata hivyo, anazielekeza taasisi wezeshi, kuondoa ukiritimba kwa wawekezaji badala yake watumie nafasi zao kuwaelekeza taratibu zinazotakiwa ili kufikia malengo waliyowekwa.

MAFANIKIO NA TAKWIMU ZA VIWANDA

Katibu Tawala Msaidizi wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji mkoani Pwani, Rehema Akida, anafafanua viwanda vimefikia 1,535 ,katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita pekee chini ya Rais Samia vimejengwa viwanda vipya 131 kati ya hivyo vikubwa na vya kati ni 122.

Ongezeko hili limechangia ajira za kudumu 18,809 kwa mwaka 2024, kutoka ajira 14,559 mwaka 2021, ajira zisizo za kudumu zimeongezeka hadi kufikia 60,000 mwaka 2024, kutoka 40,000 mwaka 2021.

Rehema anaelezea, viwanda vingi vimejengwa katika Halmashauri mbalimbali za mkoa, zikiwemo Kibaha Mji (418), Mkuranga (270), Chalinze (266), Rufiji (265), Halmashauri ya Wilaya Kibaha(137), Bagamoyo(120), Kisarawe (50), Kibiti (31 na Mafia(18).

Kati ya viwanda hivi ,(700) vinajihusisha na uchakataji wa madini, utengenezaji vifaa vya ujenzi (119), viwanda vya nyama viwili, viwanda vya vifaa vya umeme (14), madini ya vito( 25), uunganishaji magari na ufundi mbalimbali (114 )ambapo vikubwa vipo vitatu na viwanda vya dawa (17).

Maeneo maalum ya uwekezaji kutoka 17 kwa mwaka 2021 hadi kufikia maeneo 26 yanayotarajiwa kujenga kongani, huku kongani tano kubwa zikitarajiwa kutoa ajira zaidi ya 7,050.

WAWEKEZAJI NA MAENDELEO YA VIWANDA

Ruby Zhu, Ofisa Biashara wa kiwanda cha vioo cha KEDA Tanzania, anaeleza kuwa kiwanda hicho, kinachojengwa Mkuranga, kitagharimu dola za Kimarekani milioni 309, sawa na sh. bilioni 803.4 za Tanzania.

“Kiwanda hiki kitazalisha tani 600 za vioo kwa siku na tani milioni 219 kwa mwaka, na kitatoa ajira zaidi ya 1,600,”Zhu anafafanua.

Charles Bilinga, Mkurugenzi wa Afriq Engineering and Construction Co. Ltd, anaeleza kuwa mradi wa Modern Industrial Park utagharimu takriban trilioni 3.5 na utatoa ajira za moja kwa moja 30,000.

Ofisa Fedha na Masoko wa Turnkey Real Estate Tumaini Kabengula, kampuni ambayo inahusika na mauzo na masoko na kuingia mkataba wa kutafuta wawekezaji kwenye viwanja 202 ndani ya Kongani ya KAMAKA anasema, wawekezaji zaidi ya 55 kutoka nje ya nchi wameonesha nia ya kuwekeza .

Kabengula anataja changamoto za barabara na vivutio vya kodi, zinahitaji kushughulikiwa ili kongani kama hii iweze kushindana katika soko la ndani na nje.

Kuhusu Kongani ya SINOTAN, Mratibu wa mradi wa Kongani ya Sinotan Jensen Hung anaelezea, wanatarajia kujenga viwanda vya kati na vikubwa 300 na kutoa ajira za moja kwa moja 100,000.

MAONI YA WANANCHI

Amina Saleh, mkazi wa Loliondo,Kibaha anahimiza viwanda kutoa ajira zaidi kwa vijana wazawa, hasa kwenye nafasi za ofisini, badala ya ajira za muda.

Saidi Ally Mtina kutoka Mailmoja anaeleza kuwa licha ya Mkoa wa Pwani kuwa na viwanda vingi, bado ni kati ya mikoa maskini nchini, kulingana na ripoti ya NBS ya mwaka 2022.

Anaomba serikali iongeze ajira na kuongeza nguvu katika uzalishaji ili kuinua pato la mkoa.

WIZARA YA VIWANDA

Waziri wa Viwanda na Biashara, Alhaj Dkt. Selemani Jafo, amewahakikishia wawekezaji kuwa Tanzania ni nchi salama kwa uwekezaji wa viwanda.

Serikali imejipanga kutoa ushirikiano wa karibu kwa wawekezaji na kutatua changamoto zao, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Rais Samia katika kukuza sekta ya viwanda.

Kadhalika, utekelezaji wa Programu ya Viwanda ya 2025-2030 una lengo la kila mkoa kuanzisha viwanda vikubwa, vya kati, vidogo, na vidogo sana ili kuongeza ajira na kukuza uchumi.

HITIMISHO
Mafanikio ya Mkoa wa Pwani katika sekta ya viwanda yanaonyesha mchango mkubwa wa serikali na sekta binafsi.

Ili kuendeleza mafanikio haya, ni muhimu serikali iendelee kuboresha mazingira ya uwekezaji na kushughulikia changamoto zilizopo.

Mkoa wa Pwani una nafasi nzuri ya kuwa kitovu cha viwanda nchini, na jitihada za sasa zikiimarishwa, Tanzania inaweza kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.