Iran imeishambulia Israel kwa makombora kadhaa na kuongeza joto katika mzozo wa miezi kadhaa baina ya Israel na makundi yanayoungwa mkono na Iran ya Hamas na Hezbollah.

Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari amesema shambulizi la makombora kiasi 180 lililofanywa na Iran jana Jumanne lilinuia kuwaua maalfu ya raia wa Israel na halikuwa la kawaida na wala halikutarajiwa.

Jeshi la Israel pia limelilaani shambulizi hilo likiliita kuwa ongezeko baya na la hatari la machafuko.

Hagari amesema Iran na washirika wake wanataka kuingamiza Israel na kutakuwa na matokeo na hatua za kujibu shambulizi hilo.

Rais wa Marekani Joe Biden amesema Marekani inaiunga mkono kikamilifu Israel kufutia shambulizi hilo la makombora ya masafa marefu, akilieleza kuwa limeshindwa na lisilo na tija yoyote.

Akizungumza na waandishi habari katika ikulu yake mjini Washington, Biden amesema kuna mazungumzo yanayoendelea kuhusu jinsi Israel itakavyojibu shambulizi la Iran na kwamba athari kwa serikali ya mjini Tehran zitaonekana. Biden amesema atazungumza na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Please follow and like us:
Pin Share