Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeanza mpango muhimu wa kutoa huduma ya upimaji wa magonjwa ya moyo bure mkoani Geita, unaolenga wakazi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Kambi hiyo ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo inayoanza leo inakwenda sambamba na Maonesho ya 7 ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea kesho hadi Oktoba 13 mkoani Geita na ni sehemu ya shughuli za JKCI katika kuadhimisha Siku ya Moyo Duniani.
Kambi hiyo inalenga kutoa uchunguzi wa kina wa magonjwa ya moyo na mishipa kwa watu binafsi katika Kanda ya Ziwa, eneo ambalo huduma maalum za afya ya moyo ni chache.
Mpango huo ni hatua madhubuti ya kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wa magonjwa ya moyo nchini Tanzania, hasa katika maeneo yenye uwezo mdogo wa kupata huduma za afya za hali ya juu.