Na Isri Mohamed

Aliyewahi kuwa mshambuliaji wa Yanga SC, Fiston Mayele amesema kama itatokea akarudi kucheza kwenye Ligi Kuu ya Tanzania basi atarudi klabu ya Yanga kwani ndio nyumbani licha ya maneno maneno yaliyotokea hapo nyuma baada ya kuondoka kwake.

Mayele ameyasema hayo katika uwanja wa Azam Complex Chamazi baada ya kutazama mchezo wa Yanga vs KMC uliomalizika kwa wananchi kuvuna alama tatu kwa ushindi mwembamba wa bao moja lililofungwa na Maxi Nzengeli.

“Yale za zamani yameshapita, wananchi nimewamiss sana na ndio maana leo nimekuja kuangalia gemu na nimefurahi mmenipokea vizuri, na kuhusu kurudi kucheza tena Yanga tuseme Inshaalah”

Aidha Mayele amemuelezea mchezaji Maxi Nzengeli ambaye ni raia mwenzake wa Congo kuwa atazidi kufanya vizuri Yanga.

“Nilimwambia Injinia Hersi kabla ya mechi kuanza kwamba Maxi ndiye atakayefunga goli la kwanza, nimecheza nae timu ya taifa michuano ya Chan, alikuwa anacheza namuona kwa uchezaji wake na ligi ya Tanzania ataendelea kufanya vizuri, hachoki, anakaba sana na kuchezesha timu, ana quality nzuri”

Please follow and like us:
Pin Share