Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete ameongoza ameongoza maadhimisho ya kampeni juu ya kukabiliana na changamoto ya afya ya akili.

Shughuli za maadhimisho hayo zimefanyika leo hii Septemba 28 katika viwanja vya Gymkhana, Posta, Dar es Salaam.

Kampeni hiyo pia imeenda sambamba na maadhimisho ya miaka 27 ya utoaji huduma kwa blBenki ya Exim Tanzania.

Kampeni hiyo imefanyika mwaka huu ikiwa ni msimu wake wa pili ambapo waandaji wakuu ikiwa ni Benki ya Exim Tanzania kwa kushirikiana na kampuni mbalimbali zinazojishughulisha na utoaji wa bima za afya.

Akizungumza leo hii wakati wa hafla ya shughuli hizo Waziri Ridhiwani ameipongeza benki ya exim kwa jitihada zake zinazofanywa kuendelea kuboresha huduma za afya nchini kupitia mpango wake wa kusaidia jamii ujulikanao kama Exim cares.

Waziri ametoa sifa za kipekee kwa benki hiyo pia kwakuwa mstari wa mbele kusaidia katika kuimarisha huduma ndani ya sekta ya afya katika mikoa mbalimbali nchini.

“Naomba nichukue fursa hii kutambua na kuwapongeza benki ya exim kwa jitihada zenu za kuendelea kuboresha huduma za afya nchini kupitia mpango wenu wa kusaidia jamii unaojulikana kama “Exim Cares”

“Benki ya exim imekuwa mstari wa mbele kusaidia katika kuimarisha huduma ndani ya sekta ya afya katika mikoa mbalimbali nchini. Sisi kama serikali tunatambua mchango wenu mkubwa katika kuboresha huduma za muhimu kwa maendeleo ya jamii inayowazunguka” amesema.

Aidha waziri ameunga mkono tamasha hilo ikiwa miongoni mwa malengo yake ni kukusanya kiasi cha fedha ndani ya miaka mitatu ijayo ili kusaidia kuboresha miundombinu na huduma za afya kwa ajili ya watanzania wenye matatizo ya afya ya akili.

“Leo kupitia tamasha la Exim bima festival 2024 naunga mkono tamasha hili lenye lengo la kukusanya jumla ya shillingi milioni 300 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ili kusaidia kuboresha miundombinu na huduma za afya kwa ajili ya ndugu zetu wenye matatizo ya afya ya akili.”alisema.

Kwa upande mwingine pia Benki ya Exim Tanzania kupitia Afisa mtendaji mkuu wake Jaffari Matundu amelielezea tamasha hilo kuwa ni sehemu ambayo wamedhamiria kuchochea mtazamo chanya kwa watu wanaokabiliana na changamoto za afya ya akili.

“Mwaka huu ikiwa ni awamu ya pili ya tamasha hili, bado tupo katika sekta ya afya huku tukiongozwa na kauli mbiu ya ,Amsha Matumaini, tumedhamiria kuchochea matumaini na mtazamo chanya kwa watu wanaokabiliana na changamoto za afya ya akili. Tukisisitiza kukuza hisia ya uwezekano wa kupona, ukuaji wa kibinafsi, na maisha bora ya baadaye”

“Na ili kutimiza dhamira yetu, kupitia tamasha hili, tunategemea kuboresha ama kuongeza idadi ya vituo vya wagonjwa wa afya ya akili nchini kutokana na ukubwa wa tatizo” amesema afisa Matundu.

Kwa mujibu wa maelezo ya afisa Matundu ameeleza kuwa zoezi hilo ni zoezi endelevu ambapo litaendelea mpaka lengo litimie ambapo pia amesema kuwa kampeni hiyo imekuwa ikiendeshwa kwa zaidi ya mwezi mmoja ikiwa imewahusisha wateja wa benki hiyo , wadau mbalimbali na umma kwa ujumla wake.

Kampeni hiyo imeendeshwa leo hii huku ikihusisha baadhi ya michezo mbalimbali ikiwemo mechi za mpira wa miguu pamoja na burudani nyingine mbalimbali.

Please follow and like us:
Pin Share