Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Jumuiya ya waendesha baiskeli ijulikanayo kama Twende Butiama imepanga kumuenzi hayati Mwalimu Julius Nyerere kupitia ya Kampeni Kuendesha Baiskeli.

Maadhimisho hayo ya kumuenzi hayati Nyerere yanafanyika mwaka huu ikiwa ni msimu wake wa sita tangu yalipofanyika kwa mara ya kwanza 2019 ambapo mara zote yanahusisha msafara wa waendesha baiskeli kutoka jijini Dar es Salaam kwenda katika kijiji cha Butiama.

Maadhimisho hayo yamelenga kuyaenzi mazuri na jitihada zilizofanywa na hayati mwalimu Julius Nyerere katika kupigania uhuru wa taifa pamoja na kusaidia mataifa jirani katika kupigania uhuru wao.

Akizungumza na Jamhuri Digital leo hii katibu mkuu wa klabu ya waendesha baiskeli hao Salum Miraji amesema kuwa kwa mwaka huu wamelenga kumuenzi hayati Nyerere kwa namna ya kitofauti zaidi ukilinganisha na miaka mingine nyuma.

“Tunatarajia kuendesha kampeni yetu ya Twende Butiama tarehe 29 mwezi huu ikiwa ni sehemu ya kumuenzi hayati Nyerere.

“Kampeni hii kwa mwaka huu tumelenga kuiendesha kwa namna ya kipekee ambapo tutahusisha matukio mbalimbali ambayo yatakwenda kusaidia jamii yetu ambapo miongoni mwake kwa kushirikiana na wadhamini wetu tumelenga kugawa madawati katika shule baadhi tutakazopita ,tutagawa baiskeli zisizopungua 50 kwa watoto wa kike katika shule tutakazokuwa tunapita kwani changamoto ambazo sisi kama watanzania tunapopata nafasi ya kujitolea basi itabidi tunatakiwa kujitolea kwaajili ya kuboresha elimu yetu ya msingi.

“Pia kwa kushirikiana na wadhamini wetu tumelenga kuendesha shughuli za upandaji miti katika baadhi ya maeneo tutakayokuwa tunapita” amesema.

Kampeni hiyo ya twende Butiama inatarajiwa kuzinduliwa Jumamosi hii ya Septemba 28 katika makazi ya mwalimu Nyerere yaliyoko Msasani, Dar es Salaam na kuanza rasmi Jumapili ya Septemba 29 katika viwanja vya Posta vilivyoko Kijitonyama, Dar es Salaam.

Please follow and like us:
Pin Share