Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inajipanga kujenga uwanja mkubwa wa michezo utakaokuwa na vigezo vinavyokubalika na Shirikisho la Soka Duniani FIFA pamoja na Shirikisho la Soka Barani Afrika CAF.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipokutana na viongozi na wachezaji wa Klabu ya Simba ya Dar es Salaam waliofika kumsalimia kabla ya mchezo wao wa kesho dhidi ya Azam utakaochezwa Uwanja wa Amani Complex, majira ya saa mbili usiku.

Alisema, lengo la Serikali ni kuhakikisha michuano ya soka inayowashirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) na ile michuano ya soka ya mataifa ya Afrika kwa timu za taifa (AFCON), kuwa Zanzibar ni sehemu itakayochezwa michezo hiyo.

Amesema, Zanzibar imefanikiwa kwenye maeneo mbalimbali ya utalii ikiwemo utalii wa fukwe, urithi na makumbusho, hivyo wakati umefika kwa Serikali na wadau wa utalii, kuangalia maeneo mengine ya kuutangaza utalii ikiwemo sekta ya michezo.

Halikadhalika, alisema Serikali inaendelea kuwekeza na kuimarisha miundombinu ya michezo kwa kuendeleza ujenzi wa viwanja vya michezo vyenye hadhi ya kimataifa kwa maeneo yote ili michuano mikubwa ichezwe Zanzibar.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameelezea dhamira ya Simba ya kujenga kituo cha kuwaendeleza vijana katika mchezo wa soka hapa Zanzibar (soccer academy) kuwa ni jambo jema na kuwaahidi Serikali ipo tayari kuwaunga mkono kwa kuwapa eneo la ujenzi wa kituo hicho.

Pia, amevitaka vilabu vya kandanda nchini kucheza michezo yao mingi Zanzibar ili kuimarisha sekta ya michezo pamoja kuinua mwamko wa vijana kupenda michezo.

Rais, Dk. Mwinyi amebainisha kuwa Zanzibar ina vipaji vingi vya vijana wanaohitaji kuendelezwa hususan kwenye soka ili kuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuzisaidia timu zao na timu za taifa.

Naye, Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu amemuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Klabu hiyo ipo tayari kuitangaza Zanzibar kimataifa kupitia utalii wa michezo.

Vilevile, amepongeza juhudi za Rais Dk. Mwinyi kuendeleza viwanja vya michezo kila wilaya Unguja na Pemba, kwani michezo ni nyezo muhimu ya kukuza umoja, furaha na upendo miongoni mwa wananchi.

Simba Sports Club hivi karibuni ilifanikiwa kuingia hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuitoa timu ya “Ahly Tripol” ya Libya na kuingia hatua ya makundi kwa mara ya saba.

Please follow and like us:
Pin Share