Waziri wa Uchukuzi , Profesa Makame Mnyaa Mbarawa ameshiriki katika Kongamano la Kimataifa la Usafirishaji Endelevu (2024 Global Sustainable Transport Forum). Kongamano hilo ambalo limekutanisha Mawaziri na Wadau wa masuala usafiri kutoka Mataifa mbalimbali Duniani, limeandaliwa na kuratibiwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kupitia Wizara ya Uchukuzi ya nchi hiyo.

Akizungumza katika hadhara ya Mkutano huo, Mheshimiwa Mbarawa ameeleza mafanikio na hatua mbalimbali ambayo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechukua katika sekta ya usafiri na usafirishaji ikiwemo utekelezaji wa miradi ya reli ya SGR, bandari na usafiri wa anga.

Aidha, katika hatua nyingine Mhe.Mbarawa, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kuonesha nia ya kuhuisha reli ya TAZARA ambapo makubaliano yake yalifikiwa tarehe 4 Septemba, 2024 wakati wa Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali katika Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika- FOCAC. Makubaliano hayo yalishuhudiwa na Marais wa Nchi za China, Zambia na Tanzania.

Katika Kongamano hilo, Waziri Mbarawa ameeleza fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya uchukuzi zinazopatikana nchini, hivyo kutumia jukwaa hilo kuwakaribisha wawekezaji wenye nia huku akiwahakikishia kuwa, Serikali ya Tanzania imeweka utaratibu mzuri wa kisera wa kushirikiana na Sekta binafsi katika kutekeleza baadhi ya miradi ikiwemo mradi Bandari na reli ya SGR ili kuwezesha kuifungua nchi zaidi kimaendeleo kupitia utaratibu wa Private Public Partnership (PPP). Hatua ambayo inaakisi mpango wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Endelevu wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2030.

Kongamano hilo linalofanyika kwa siku mbili tarehe 25 na 26 Septemba, 2024 jijini Beijing, China, Waziri wa Uchukuzi ameambatana na Viongozi na Wataalam mbalimbali kutoka Wizarani na Taasisi za Sekta ya Uchukuzi.

Please follow and like us:
Pin Share