Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Septemba 22, 2024 ni miaka 29 tangu baba yangu mzazi afariki dunia (wakati unasoma makala hii Jumanne Septemba 24, 2024 ni miaka 29 na siku 15). Baba yangu alifariki Septemba 12, 1995 akiwa na umri wa miaka 63.

Mzee Alphonce Mutalemwa Balile, alikuwa baba mzuri sana, baba mwenye upendo, baba aliyependa maendeleo. Hadi leo kwa wale wa umri wetu wa 50+ wanaendelea kumtambua kama Mzee wa Maendeleo.

Sitanii, inakaribika miaka 30 sasa, lakini zipo nyakati nikiamka najikuta kwenye lindi la mawazo. Namkumbuka Ta Alphonce. Baba alikuwa mwalimu. Amefundisha Ifunda, Malangali – Mufindi, Bukoba, Misungwi na alipanda cheo hadi kuwa Kaimu Afisa Elimu wa Mkoa wa Kagera miaka ya 1980. Kati ya maneno ninayoyakumbuka, baba aliniambia: “Mzungu aliyekuwa anatufundisha darasani, aliniita akasema ‘Alphonce, una akili sana. Maishani usikope. Tumia mshahara wako na kipato halali kufanya maendeleo’… Deoda milele hakikisha maishani una upendo. Jali maisha ya watu.”

Ingawa dunia imebadilika, mikopo ni sehemu ya maendeleo, nimezingatia wosia wake. Binafsi hadi leo sisongeshi na wala sijui jinsi ya kusongesha. Ninapowaza kuchukua mkopo, nawaza kuchukua mkopo wa biashara, mkopo wa maendeleo. Siwezi kukopa kwa ajili ya kulipa mchango wa harusi eti, nionekane na mimi wamo. Lakini kubwa zaidi, hadi leo kuna nyakati najikuta kwenye njozi nikimuwaza baba, Ta Alphonce Balile. Nawaza angekuwapo leo, angalau akatembelea nyumbani kwangu Dar es Salaam.

La pili ni hili la kupenda na kujali maisha ya watu. Na hili ndilo limekuwa kiini cha makala hii ninayoiandika leo. Nimewaza maisha ya watoto wa Ndugu Mohamed Ali Kibao aliyeuawa baada ya kushushwa kwenye basi. Nimewaza mimi kama leo baada ya miaka 29 bado tangu kifo cha baba yangu naugulia maumivu, watoto wa mzee Kibao ambao haujafika hata mwezi wana maumivu kiasi gani?

Sitanii, ni kwa kiwango hicho hicho nawaza kuwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), usoni wanaona maumivu sawa na watoto wa mzee Kibao. Mzee Kibao na CHADEMA, walikuwa familia. Wameishi pamoja. Wanashuhudia mmoja kati yao anafariki dunia. Ni maumivu. Wanamkumbuka Alphonce Mawazo, Ben Sanane na wengine. Inauma.

Ni kwa mtazamo wa kuangalia picha pana,nilipita katika mitaa ya Dar es Salaa nikaona maandalizi katika vituo vidogo vya Polisi Dar es Salaam,  wakishushwa askari 15 na kuendelea. Tena si askari wa kawaida, wanashushwa FFU. Mitaani yanapita magari ya polisi. Nimeona pia taarifa ya CHADEMA, wamepeleka taarifa Polisi Ijumaa Septemba 20, 2024 kwa ajili ya maandamano ya amani.

CHADEMA walitaka kuanzia Ilala Boma hadi Mnazi Mmoja na Magomeni hadi Mnazi Mmoja. Jambo moja tu niliseme. Sina uhakika kama kwa sasa litasikika au la, ila basi libaki katika historia. Moja, sitamani kuona watu wanakufa kifo kisichokuwa kifo cha asili. Mwaka 2000 Novemba, niliandika habari yenye kichwa cha habari: “CUF watoa siku 90.”

Baada ya hapo nilikwenda Pemba na Unguja. Chama cha Wananchi (CUF) walikuwa na kaulimbiu yao ya ‘Jino kwa Jino’. Katika habari hiyo niliyoiandika aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Tanzania Bara, Wilfred Lwakatare aliniambia na nikaandika kuwa CUF wao ni Ngangari. Baadaye nilimhoji aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Omari Mahita, akasema kama CUF ni Ngangari, wao Polisi ni Ngunguri. CCM nao wakaingia kati wakasema wao ni Nginjanginja.

Sitanii, kila uchao vyama hivi sasa vilianza kuhesabu siku kuelekea siku 90. Januari 26, 2001 ikawa kilele. Mengine ni historia. Tulizalisha wakimbizi kwenda Shimoni nchini Kenya na Chief Emeka Anyaoku wa Nigeria aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola akaja kusuluhisha. Alisuluhisha baada ya polisi na raia kadhaa kufariki dunia.

Naiona shida inapitapita. Nimesoma taarifa ya CHADEMA, inayowataarifu wafuasi wao washiriki maandamano kutoka Ilala Boma hadi Mnazi Mmoja na Magomeni hadi Mnazi Mmoja. Ukiisoma taarifa hiyo, unashawishika kuungana na CHADEMA katika maandamano haya kwa maumivu ya mauaji. Hadi naandika makala hii, sijasikia polisi wanasemaje zaidi ya ile taarifa yao yenye karibu mwezi sasa ikizuia maandamano. Sijasikia kama wamewazuia au wamewaruhusu.

Binafsi naamini tunahitaji zaidi busara kuliko nguvu. Kila upande ujipime. Polisi wakiona kweli hawa watu wanaanzia Ilala na Magomeni hadi Mnazi Mmoja, basi ikiwapendeza badala ya kuwazuia wawalinde watembee kipande hiki kifupi. CHADEMA nao nafahamu nia yao ni kufikisha ujumbe. Ni kuzuia mauaji na watu kupotea kunakoendelea. Wakiona maandamano yatasababisha watu kadhaa wengine wafariki dunia, basi maandamano haya wayaache.

Jambo moja nahitimisha nalo, nimepata fursa ya kuziona awamu zote sita. Tangu Mwalimu Julius Nyerere, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Mzee Benjamin Mkapa, Mzee Jakaya Kikwete, Dk. John Magufuli na sasa Rais Samia Suluhu Haasan. Namshukuru Mungu kwa hili. Kanisa Katoliki mwezi huu limeadhimisha Kongamanno la Ekaristi Takatifu. Kaulimbiu ilikuwa ni “Udugu Kuponya Ulimwengu, Ninyi Nyote ni Ndugu.”

Kwa hakika tunahitaji kuuponya ulimwengu na sisi sote ni ndugu. Kwamba leo hata tukigombana tukauana, mwisho wa siku tutarejea katika meza ya mazungumzo. Tunayo mifano hai kwa majirani zetu wa Kenya, Rwanda na Burundi. Wameuana, wamepigana, ila mwisho wa siku wamekaa meza ya mazungumzo kutatua matatizo yao. Nasema yanayotutenganisha ni machache kuliko yanayotuunganisha. Tuitangulize Tanzania kwanza, hili litapita, ila mauaji yakomeshwe. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827

Please follow and like us:
Pin Share