Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Naibu Kadhi Mkuu, Ali Khamis Ali amempongeza mfanyabiashara Shiraz Rashid kwa kujitolea kujenga Msikiti wa Imam Ali Bin Abu Talib eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam.

Alitoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki wakati wa hafla ya uzinduzi wa Msikiti huo hafla ambayo ilihudhuriwa na wageni mbalimbali mbali wakiwemo mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao.

Alisema lengo la kujenga Msikiti huo ni kuhudumia waumini kwenye ibada na aliwashauri watanzania wengine kuiga mfano huo kwani hiyo ni kazi ya Mungu.

“Tunatoa wito watu wengine waige mfano wa Shiraz ili tujenge nyumba za ibada kwani nyumba hizi zinasaidia kurejesha utulivu na amani kwa watu kufanya ibada, huu ni moyo wa upendo wa ndugu yetu aliouonyesha kwa hiyo natoa wito kwa wengine waige,” alisema

Naye Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Kawambwa alisema ujenzi wa Msikiti huo ni jambo jema na kuwataka watu wengine kuanzisha ujenzi kama huo kwani hiyo ni kazi ya Mungu.

“Mtume alipoingia Madina alijenga Msikiti kwanza kwa maana kwamba ile ni sehemu ya Waislamu kukutana na kujadiliana na washirikiane kufanya mambo yao pale kwa hiyo namshukuru Shiraz kwa kunialika kuja kwenye ufunguzi huu,” alisema Sheikh Walid.

Please follow and like us:
Pin Share