Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

WANANCHI mkoani Ruvuma wametakiwa kujitokeza kwa wingi kumpokea Rais wa jJamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye anatarajia kufanya ziara ya kikazi siku sita kuanzia Septemba 23, mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed wakati alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake jana mchana kuhusiana na ziara hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahamed Abbas Ahamed akizungumza na waandishi wa Habari mapema leo ofisini kwake

Alisema kuwa Rais akiwa mkoani humo matukio matatu yatafanyika ambapo tukio la kwanza atafunga tamasha la tatu la Taifa la Utamaduni ambalo kilele chake ni septemba 23 mwaka huu ambalo linafanyika katika viwanja vya majimaji Manispaa ya Songea.

Alifafanua kuwa Septemba 24 mwaka huu Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ataanza ziara ya kikazi ambapo atazitembelea wilaya zote tano za mkoa wa Ruvuma ambazo ni Mbinga,Nyasa,Tunduru,Namtumbo na Songea na kwamba atafanya shughuli mbalimbali ikiwemo kuongea na wananchi kupitia mikutano ya hadhara.

Mkuu wa Mkoa Ahmed Abbas Ahmed alisema pia Rais Dk.Samia Suluhu Hassan atazindua, kufungua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuongea na wazee wa Mkoa wa Ruvuma.

Alieleza kuwa tukio la tatu ambalo litafanyika ni kushiriki baraza la umoja wa wanawake Tanzania(UWT) Taifa linalotarajia kufanyika katika Manispaa ya Songea ambapo Rais baada ya kuhudhuria atafunga kikao hicho kinachotarajiwa kufanyika Septemba 28 mwaka huu ambacho kitahudhuriwa na wajumbe wa umoja wa wanawake wa wilaya zote hapa nchini.

“Kama nilivyosema baada ya kufungwa kwa mkutano wa baraza kuu la UWT Taifa Rais Samia Suluhu Hassan atahitimisha ziara yake mkoani Ruvuma kwa kufanya mkutano wa hadhara wa wananchi wa manispaa ya Songea katika uwanja wa majimaji ambapo atatumia mkutano huo kuongea na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma”alisema mkuu huyo wa mkoa.

Alisema kuwa ziara hiyo ni fursa kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma hivyo pamoja na mambo mengine aliwaasa kuboresha mazingira ili yawe rafiki jambo ambalo litawavutia wageni mbalimbali ambao wanatarajia kuwasili mkoani humo.

  
Please follow and like us:
Pin Share