Na Mwandishi Wetu, JammhuriMedia, Dar es Salaam

Waziri wa Afya Jenista Mhagama ameipongeza Bohari ya Dawa (MSD) kwa kuendelea kuhakikisha inanunua vifaa muhimu vinavyohitajika kusaidia kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa wakiwa njiti.

Waziri Mhagama amesema hayo leo wakati akikabidhi vifaa tiba maalumu vya kuwasaidia watoto wenye matatizo kupumua, ambavyo amevikabidhi kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Mohammed Mang’una kwa niaba ya waganga wakuu wote nchini.

Vifaa Tiba hivyo 130 vyenye thamani ya Tsh: 212,854,365 vimenunuliwa na Bohari ya Dawa (MSD) kwa kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ili viweze kusaidia kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao yaani njiti.

“Tuendelee kununua mashine na vifaa hivi kadri mahitaji ya vituo vyote vya kutolea huduma za afya yanavyowasilishwa, ili angalau kila kituo kiwe na mashine tano, kwa sababu wanaweza wakapatikana watoto watano kwa mara moja wenye matatizi tukawaokoa, tuwasaidie watoto hawa wasipoteze maisha.” amesisitiza.

Amesisitiza kuwa watoto wanaozaliwa kabla ya kutimiza muda wa kuzaliwa (njiti) kwa asilimia 80 hupata tatizo la kupumua kwa kuwa mapafu na viungo vingine vinakuwa havijakomaa na hupelekea kupoteza maisha, lakini pia wanaweza kupata maambukizi ya magonjwa mengine kwa haraka kutokana na kinga yao kuwa chini.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD, Rosemary Silaa amemweleza Waziri kuwa kwa sasa bodi hiyo ina mchanganyiko mzuri wa wajumbe ambao wana utaalamu wa maeneo yote muhimu yanayohusiana na majukumu manne ya MSD ya uzalishaji, ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bohari ya Dawa (MSD), Mavere Tukai amesema maagizo yote yaliyotolewa na Waziri wa Afya yatatekelezwa ikiwemo kuendelea na ujenzi wa maghala ya kuhifadhia dawa, mifumo ya mnyororo wa ugavi kusomana, pamoja na kuendelea na uzalishaji wa bidhaa za afya utazingatiwa.

Please follow and like us:
Pin Share