Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padri Dkt. Charles Kitima, leo Jumapili Septemba 15, 2024, kwenye kilele cha Kongamano la 5 la Ekaristi Takatifu Kitaifa, amewatambulisha kwa waumini viongozi wa kisiasa akiwemo Katibu Mkuu wa CCM, Emmanuel Nchimbi, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA – Bara, Tundu Lissu, na Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika. Akiwasimamisha pamoja mbele ya umati uliokusanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Padri Kitima aliwatambulisha kila mmoja kwa ufupi na kusisitiza umuhimu wa upendo miongoni mwao.

Padri Kitima alisisitiza mara kwa mara kuwa, “Ninyi nyote ni ndugu, mkaishi kwa upendo,” na kuwataka viongozi hao wa kisiasa kupeleka tunu za Injili na kusambaza upendo ndani ya vyama vyao. Aliwataka waonyeshe mfano wa umoja na upatanisho kwa jamii wanayoiwakilisha.

Tukio hili limehudhuriwa na maelfu ya waumini wa Kanisa Katoliki kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, wakiongozwa na Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa.

Aidha, Padri Kitima alikumbuka tukio la mwaka 2017 alipokwenda Nairobi kumtembelea Tundu Lissu aliyekuwa akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi, akibainisha kuwa hadi leo haijulikani sababu ya tukio hilo.

Please follow and like us:
Pin Share