Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe Dkt Benson Bagonza amesema ifike hatua nchi iwe na mfumo unaotoa uhuru wa kupiga kura na kuchagua na siyo kama ilivyo sasa ambapo mfumo unaruhusu kupiga kura na siyo kuchagua.

Dkt Bagonza amesema kwa sasa Taifa limeingia gizani kutokana na watu kupotea na kuuawa na eneo lililoathirika zaidi ni eneo la demokrasia kwani wananchi wana mashaka juu ya kesho yao kutokana na kukosekana kwa uhuru wa kutoa maoni binafsi.

Akizungumza katika hafla ya usiku wa kufunga Wiki ya CSO jijini Arusha, ameitaka serikali kuwa makini na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyoendelea nchini ili kuondoa mashaka na hasira mioyoni mwa watu.

“Kwa Sasa mfumo umechezewa kwani waliochaguliwa wapo juu kuliko waliyewachagua, mfumo unamruhusu mtu kutoa mawazo yake lakini siyo kumhakikishia ulinzi wake lakini pia mfumo umeimarisha mashaka ya kudumu kwa watu wote” amesema Askofu Dkt. Bagonza.

Hata hivyo Askofu Dkt Bagonza ameikumbusha serikali kuiishi falsafa ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya Maridhiano, Mabadiliko, Ustahimilivu na Kujenga (4R) ambayo ina lengo la kujenga amani na utulivu nchini na kuleta maendeleo ya kudumu.

Hata hivyo amesema tunu ya amani ya nchi iliyoachwa na waasisi wa nchi hii inatakiwa kulindwa na kutunzwa, pasipo kuingiliwa na nguvu ya mhimili wowote.

“Hatuwezi kuendelea hivi ikiwa hakuna na Demokrasia huru, na ninaogopa sana vurugu za wasio na matumaini kuliko wenye madaraka…..imefikia wakati wanasiasa wa chama kilichoko madarakani hawako huru kutoa maoni kukosoa wanapoona mambo hayaendi sawa, wanasiasa wa vyama vingine nao wanaogopa kutoa maoni yao “amesema Dkt. Bagonza na kuongeza.

“Hata nyie AZAKI mna hofu kutoa maoni yenu juu ya mwenendo wa nchi, hii ni hatari na giza kwa kesho yetu, hakuna serikali isiyokosolewa duniani kote, hii inasaidia kuwakumbusha wajibu wao na sio kuwaogopa” ameeleza Dkt.Bagonza.

Rais wa AZAKI Dkt.Stagmata Tenga amezitaka taasisi zote nchini kuendeleza ushirikiano katika kuongoza jamii ili ziwe imara na rasilimali watu wenye uwezo na kuelewa haki na utu wao.

Please follow and like us:
Pin Share