Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha

Kwa miongo kadhaa wanawake kutoka jamii za pembezoni ikiwemo ya kimaasai wamekuwa hawapewi kipaumbele kwenye masuala mengi kama elimu, uongozi na kiuchumi.

Kutokana na changamoto hizo, serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali ya ndani na nje ya nchi yameweka jitihada ili kumkomboa mwanamke na mtoto wa kike kwa kutunga sera za ushirikishwaji pamoja na kutoa elimu.

Wakizungumza kwenye kigoda cha mwanawake katika wiki ya AZAKI leo katika Kata ya Kimokowa wilayani Longido mkoani Arusha, Mwenyekiti wa vikundi zaidi ya 300 vya maendeleo wilayani humo Nambori Nabak amesema kupitia elimu waliopata kutoka Shirika la Legal Services Facility (LSF) imewasaidia wanawake kujua haki zao na kuzidai lakini pia wanaume wamekuwa mstari wa mbele kuunga mkono jitihada hizo.

“Hapo mwanzo kila mtu ni shahidi ya kile kilichokuwa kinaendelea kwenye jamii yetu, kulikuwa hakuna usawa kabisa, lakini Leo ninavyozungumza siyo wanawake wamehamasika tu, bali wanaume nao wanatuunga mkono” alisema Nabak na kuongeza

“Leo wanaume wanatekeleza masuala ya wanawake, tena wazee wa mila wamekuwa vinara wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto, pia akina baba wamejiunga vikoba, huu ni ushindi mkubwa sana kwenye jamii yetu” Nabak

Hata hivyo kiongozi wa mila kutoka jamii hiyo, Laigwanani Lucas Sambeke amesema wamehamasika na kuelimika na pia wanaendelea kuelimisha jamii juu ya haki za wanawake katika nyanja zote za maisha suala ambalo limepewa mwitikio mzuri.

“Hapo awali tuliwasisitiza wanawake kuwa majukumu yao ni yale ya ndani ya familia tu na siyo nje ya hapo, lakini baada ya kupewa elimu hii na kuitekeleza, tunashuhudia wanawake viongozi, wafanyabiashara na wanamiliki rasilimali kama ardhi na wakati huo huo wanaendelea kutekeleza majukumu yao ndani ya familia zao” alisema Laigwanani Sambeke.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Eworendeke, Esupath Laiza amesema serikali imetunga sera inayotaka mwanamke kushirikishwa kwenye kila jambo ndani ya jamii hivyo kuitaka jamii kuendelea kuwamahasisha wanawake kujitokeza.

Amesema wamekuwa wakishirikiana na mashirika yaliyopo wilayani hapo kutoa elimu ya madhara ya ukeketaji, haki za wanawake na pia tunatoa elimu kwa wazazi ya namna bora ya kulea mtoto kwani mtoto anategemewa kuwa viongozi bora wa kesho ndani ya jamii” amesema Laiza.

Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Longido, Upendo Ndorosi amesema wanawake wanaendelea kuhamasika na tayari ameshawajengea uwezo wanawake 11 kwa ajili ya kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa.

Mkurugenzi wa shirika LSF Lulu Mwanakilala akizungumza kwenye kigoda cha hicho amesema shirika hilo limejikita katika utoaji wa elimu ya haki za binadamu hususani kwa wanawake na watoto, haki zao kiuchumi, haki zao kisiasa, afya pamoja na kutoa elimu ya kupambana na ukatili wa kijinsia.

Please follow and like us:
Pin Share