Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

DIWANI wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam, Beatrice Edward amewataka vijana kutumia mitandao kujinufaisha na wala sio katika mambo yasiyokuwa na faida.

Ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye Jukwaa la Usimamizi wa Mtandao Tanzania Internet Governance Forum(TzIGF) liliondaliwa na Taasisi ya Internet Society Tanzania Chapter(ISOC-TZ).

Amesema vijana wengi wamekuwa wakijihusisha na matumizi mabaya ya mitandao jambo ambalo limekuwa likipelekea mmomonyoko wa maadili katika jamii.

“Kipekee nitoe shukrani kwa walioandaa kongamano hili, kwani ni la muhimu sana kwa vijana na watanzania kwa ujumla. Kama mnavyoelewa, kwasasa nchi yetu tunaishi kwa kutegemea mitandao…na mitandao inaweza ikakufanya kunufaika kama utaitumia vizuri na inaweza ikakufanya ukaharibikiwa kama utaitumia vibaya.

“Sisi kama watunga sera na watunga Sheria za Nchi tunatoa wito kwa vijana kuendelea kutumia mitandao katika manufaa. Na vijana wengi tumeona wanaitumia mitandao kwa mihemko na hawaitumii kama jukwaa la kuweza kumtoa sehemu moja kwenda nyingine kwa maana ya kumfanya aweze kufikia ndoto zake kupitia mtandao,” amesema Beatrice.

kwa upande wake, Mhandisi Danford Mbarama kutoka Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, amesema Serikali katika kusapoti jambo hilo, imejikita katika kujenga miundombinu ambapo hadi sasa Faiba imeweza kusambaa katika sehemu mbalimbali za nchi.

“Serikali inahakikisha wilaya zetu zinafikiwa na mfumo huu wa Faiba ili kurahisisha mawasiliano kwa wananchi.
Kwahiyo nawashauri vijana waweze kujifunza namna mbalimbali ya matumizi ya intaneti kwa kufanya hivyo itakuwa ni msingi mzuri wa kuboresha maendeleo ya nchi yetu.

Mdau wa masuala ya Mtandao, Miriam Shaka amesema “Vijana tunahitaji sapoti kwa kupata sera na kanuni ambazo zitasaidia kufika mahali pazuri kwenye masuala ya kimtandao ambapo mambo mengi yanaweza kufanyika kwa kutumia mtandao,”.

Naye Mratibu wa Jukwaa hilo, Nazar amesema linafanyika kwa mara ya 11 tangu kuanzishwa kwake, ambapo limewakutanisha wadau mbalimbali kujadili masuala ya kimtandao.

“Mkutano huu ambao ulianza jana, kwa kuwapa mafunzo vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 kwa maana ya kuwawezesha waweze kuwa viongozi wanaojitambua na kuelewa juu ya jukumu la kusimamia mtandao wa intaneti.

“Kama mnavyojua mtandao wa intaneti ni mkusanyiko wa mitandao mingi duniani, jukwaa hili lengo kuu ni kuwakutanisha wadau ambao wanazungumzia na kujadiliana mada mbalimbali zinazohusu usimamizi wa intaneti kwa upande wa Tanzania. Na wadau hao ni pamoja na serikali, watu wa elimu ya juu, sekta binafsi, vyama visivyo vya kiserikali, pamoja na wataalamu wa Tehama,” amesema.

Amefafanua kuwa jukwaa hilo wajadili masuala mbalimbali ikiwemo sera na Sheria na baada ya hapo watatoa ripoti pamoja na maoni ambayo yataweza kusaidia kwenye mtandao ambao utakuwa bora.

Please follow and like us:
Pin Share