Nguvu na Mamlaka ya Umma ni maneno matano yanayobeba dhana pana ya falsafa ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA.  Kwa wale ambao kwa bahati mbaya au hata kwa makusudi ni wavivu wa kufikiri, wazo au hata matumizi ya misuli siyo maana wala lengo la falsafa hiyo.

Katika makala haya napenda ieleweke na kuzingatiwa kuwa Nguvu na Mamlaka ya Umma lengo na wazo kuu kama tutakavyoona hapo baadaye ni hali ya kutosigana baina ya viongozi na wale wanaowaongoza. Nimeshawishika kukubaliana na maelezo ya neno “Philosophy” kwa lugha ya Kiingereza. Maneno yanayohusika yanasomeka hivi, “The idea that you should treat others as you would like them to treat you is a fine philosophy of life” Longman Dictionary of Contemporary English.  Maandishi haya yanapatikana ukurasa wa 1301.


Suala la uhusiano baina ya viongozi na wanaoongozwa limewekwa bayana katika Katiba ya nchi yetu ya mwaka 1977.  Tuanze na misingi ya Katiba inayopatikana katika utangulizi; “kwa kuwa sisi Wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani; na kwa kuwa misingi hiyo yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye demokrasia ambayo serikali yake husimamiwa na bunge lenye wajumbe waliochaguliwa na linalowawakilisha wananchi,……….” Utangulizi huu usomwe pamoja na ibara ya 8.(1)(a).  “8 (i) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii na kwa hiyo…


(a)   Wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa katiba hii”.


Tujaribu kufikiri tukijiuliza na kutafakari katiba ni kitu gani. Mtu anaweza kusema katiba ni jumla ya mkusanyiko wa utashi wa jamuiya ya watu, wa namna na utaratibu wanaojiwekea wa jinsi gani waendeshe maisha yao kiuchumi, kijamii, kisiasa na hata kiutamaduni.  Jenerali Ulimwengu hupenda kueleza kuwa katiba iakisi “ethos” ya jamii inayohusika, kwa mfano jamii ya Watanzania.  Ufafanuzi wa neno “ethos” katika kamusi niliyorejea hapo awali ukurasa wa 575 inasomeka hivi, “e-thos the set of ideas and moral attitudes that are typical of a particular group; a community in which people lived according to an ethos of sharing and caring”. Tuseme kwa muhtasari, Katiba ni mali ya wananchi wenye nchi yao . Katiba si kinyume cha hapo na kamwe haiwezi kuwa hadhi ya chama cha siasa kilichopewa dhamana ya kuunda serikali.


Turudi kwenye mada ya makala haya. Nimeeleza nionavyo mimi kuwa chimbuko la Nguvu na Mamlaka ya Umma ambalo ni utashi wa watu wenyewe unawekwa kimaandishi katika katiba. Maelezo na ufafanuzi wake ukoje?  Ibara ya 3.1 ya Katiba ya CHADEMA inatoa jibu kwa kusema hivi; “3.1 Falsafa ni fikra na mtazamo wa chama ambayo ni kuamini katika “Nguvu na Mamlaka ya Umma” (The People’s Power) katika kumiliki, kuendesha, kubuni na kuendeleza uamuzi, mawazo, rasilimali, uchumi na siasa ya nchi yao ”.


Aidha, maneno, “Umma ndiyo wenye madaraka ya mwanzo na mwisho katika kuamua hatma ya nchi na taifa pasipo kuingiliwa, kudanganywa au kughilibiwa na viongozi, watawala au wageni”, yanasema kila kitu.


Uko ukweli katika msemo, mazoea yana tabu. Leo hii kwa watawala wetu hakuna wazo au kuamini kuwa Nguvu na Mamlaka ya Umma ndiyo njia ya msingi ya kubadilisha fikra na uongozi (utawala) unaokandamiza umma ili kuibua fikra mpya kwa watawala na watawaliwa na kuweka uongozi unaoweza kumilikiwa, kuhojiwa na kuwajibishwa na umma kwa kutumia vyombo vilivyopatikana kwa utashi wa wengi kupitia uchaguzi huru na wa haki. Kwa kifupi ikubalike kwa mfano mimi, wewe na yeye tusikwepe wajibu wa kuhoji mambo ya umma yanapokwenda kinyume na matarajio ya wengi.


Aidha, miongoni mwa jamii ya sisi sote baadhi ya wale tuliowakabidhi dhamana ya uongozi kwa niaba yetu, wakubali kuwa tunapowahoji kuhusu utekelezaji wa mambo tuliyokubaliana kwa manufaa na maslahi yetu wote, wakubali, watambue na kujiona wanawiwa kutoa maelezo ya kuridhisha.


Kamwe wasikimbilie kinga ya ngao iliyotengenezwa kwa magamba ya mayai ya kuku wa kisasa! Hakuna wa kunihoji mimi mkubwa. Lakini ikumbukwe mkubwa ni Mwenyezi Mungu peke yake, wengine wote ni watumishi tu.


Vichwa ngumu wa dhana ya kiongozi kuwa mtumishi niwakumbushe.  Kwa wafuasi wa Kristo; Kristo mwenyewe aliwaambia mitume wake akisema, “Nimekuja kutumikia na siyo kutumikiwa”. Katika nyanja ya siasa tujikumbushe hotuba ya kwanza ya mwasisi wa Taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mara tu baada ya kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika mwaka 1961.


Mwalimu alisema, “Nawaelezeni jambo hili kwa unyenyekevu mkubwa, kwa sababu mimi na wenzangu ni watumishi wenu ninyi, ninyi mnaonisikiliza. Tunajua kuwa mnatuamini nanyi tunawaamini. Na ni ninyi tu mnaotupa nguvu zetu tunazozihitaji kwa kazi kubwa iliyo mbele yetu. Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na imani mliyo nayo juu yetu, tunapata na tunazidi kupata nguvu za kuendesha serikali yenu. Na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu tutajitahidi kuwatumikieni bila ya kujitafutia faida zetu wenyewe au fahari ya cheo”.


Sijui zama zetu hizi ni watawala wangapi wanajikabidhi kwa Mungu katika kutekeleza wajibu wao kwetu watawaliwa katika kuendesha serikali; chombo chetu wananchi. Wangapi hawajitafutii faida binafsi kwa hasara ya umma?  Na hivi ni kweli hawajitafutii fahari ya cheo, huku wakisahau kuwa cheo ni dhamana waliyokabidhiwa na sisi wenyewe? Binafsi naikubali ibara ya 3.8 katika Katiba ya CHADEMA. Inasema, “Falsafa ya Nguvu na Mamlaka ya Umma inalenga kuwaamsha, kuwahamasisha, kuwashawishi na kuwaandaa Watanzania wachukue hatua ya kumiliki, kuitawala, kuilinda na kuifaidi nchi yao tofauti na kipindi cha miaka mingi chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa na miaka kumi na nne ya mwanzo wa mfumo wa vyama vingi”.


Nimnukuu Mwalimu Nyerere aliposema, “Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu” utekelezaji wa misingi na ufafanuzi wa maudhui ya falsafa ya Nguvu na Mamlaka ya Umma kwa vitendo utatuhakikishia haki na amani katika jamii yetu Watanzania. Uelewa kuwa falsafa hiyo hailengi matumizi ya nguvu kama itegemewayo kwa watu au majitu ya miraba minne, bali matumizi ya elimu, weledi, hamasa na kutimiza wajibu wa kila mmoja wetu katika nafasi ya dhamana yake katika jamii yetu Watanzania. Sioni kwa nini haki na amani visitamalaki katika nchi yetu kama lengo la falsafa ya Nguvu na Mamlaka ya Umma inavyolenga.


Haki na amani ni mapacha walioungana na kwa hao wawili upasuaji wowote wa kuwatenganisha ni kifo kwao. Mapacha wetu haki na amani ni kulwa na doto, bukuru na toyi au waiswa na kato.  Kulwa hufuatiwa na doto.  Katika jamii inapotendeka haki amani hufuatia na kutamalaki. Hakuna mapambano tuyajuayo yanayoharibu amani.  Yatakuwapo mapambano ya fikra kuidhatiti hali ya kutenda haki na kudumisha amani itamalaki.


Katika gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,  Novemba 28, 2012, Mwalimu Mkuu wa Watu amezungumzia na kugusia “salamu” mbalimbali za baadhi ya vyama vya siasa.  Nikiri, labda kwa ujuzi wangu mdogo wa lugha ya Kiswahili, mifano aliyotumia Mwalimu Mkuu wa Watu si salamu, bali kaulimbiu.  “Hakiiii” jibu “Haki sawa kwa wote”; “Peoples Power” na “Asalaam Aleikum” hii ya mwisho si kaulimbiu ya chama chochote cha siasa.  Naamini ni maneno ya Kiarabu yakimaanisha “amani iwe kwenu”.


Warumi wangesema pax sit cum vobis maana ni ile ile ya “amani iwe kwenu”. Kaulimbiu hizi Mwalimu Mkuu wa Watu amezitolea maelezo sahihi kama vile “salamu hii inakiri kuwa haki haitendeki ipasavyo katika nchi”; “…Wapo watu katika nchi moja ambao hawatendewi haki na wenzao; “Hawa wanahamasisha nguvu ya umma itumike kuwalazimisha wale ambao walipaswa kutenda haki, lakini hawatendi ili watende haki”.


Anahitimisha kwa kusema, “Kwa kuwa haki haiombwi, basi mapambano huwa ni lazima katika mazingira kama haya”. Mapambano kutokea hakuna budi.  Lakini si mapambano ya nguvu za misuli.


Falsafa ya Nguvu ya Mamlaka ya Umma inaharamisha matumizi ya nguvu za misuli.  Fikra na mtazamo pamoja na kuamini katika kumiliki, kuendesha, kubuni na kuendeleza uamuzi, mawazo, rasilimali, uchumi na siasa ya nchi yao wenye nchi si wito wa vita ya wenyewe kwa wenyewe.  Ukiongeza maneno “…Inalenga kuwaamsha, kuwahamasisha, kuwaelimisha, kuwashawishi na kuwaandaa Watanzania wachukue hatua ya kuimiliki, kuitawala, kuilinda, kuifaidi nchi yao tofauti na kipindi cha miaka mingi chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa na miaka kumi na nne ya mwanzo wa mfumo wa vyama vingi”,  hili si baragumu la kushika silaha tayari kupigana vita.


Wasanii wameimba, ‘Uso umeumbwa na haya’. Ni kweli wapo baadhi ya viongozi, bila haya wala soni, wanakengeuka ukweli na maudhui ya maneno hayo ya wasanii. Falsafa ya Nguvu na Mamlaka ya Umma inapowaandaa Watanzania “…Kubadilisha fikra na uongozi unaokandamiza umma ili kuibua fikra mpya na kuweka uongozi unaoweza (unaokubali) kumilikiwa, kuhojiwa na kuwajibishwa na umma kwa kutumia vyombo vilivyopatikana kwa utashi wa wengi kupitia chaguzi huru na za haki”.


Kaulimbiu alizotaja Mwalimu Mkuu wa Watu pamoja na baadhi ya ufafanuzi ulio sahihi unakidhi na kulenga kuwakumbusha wapotofu kuona haya na kujirudi. Njia ya kidiplomasia hiyo, la sivyo matumizi ya vyombo rasmi vilivyopatikana kwa utashi wa wengi kwa njia ya uchaguzi usioruhusu kumkufuru Mungu kwa wanaotangazwa washindi kumbe ni washindi katika kuiba kura.


Umma utimize na kutekeleza litakiwalo na jamii. Kabla ya kuhitimisha makala haya ngoja nimchokoze Mwalimu Mkuu wa Watu.  Lengo langu ni kujifunza zaidi kutoka kwake.  Ukimchokoza mwalimu kifikra, unafaidi somo la nguvu kutoka kwake.


Katika kaulimbiu alizochagua kutolea mfano, sijasoma kaulimbiu ya “chama tawala daima” au “ina wenyewe na wenyewe ndiyo sisi”. Yaelekea kutawala kunafutilia mbali suala la uongozi. Si ajabu lengo mojawapo tena lenye kipaumbele cha kwanza ni kushinda katika uchaguzi wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa nchini pote.

Sina hakika kama lengo hilo madhumuni yake ni kuongoza kwa kuwatumikia Watanzania au ni kutawala ili kujitafutia faida zao wenyewe na fahari ya cheo. Mambo hayo Mwalimu Nyerere aliyakemea na kuyakataza kwa nguvu zake zote.


Nihitimishe makala haya, ambayo ni maoni yangu na haki yangu kikatiba, kama ifuatavyo:  Naamini kwa dhati kabisa kwamba utekelezaji kwa vitendo wa falsafa ya nguvu na mamlaka ya umma ni mhimili wa haki na amani endelevu katika jamii. Amani ni tunda la haki.  Kutotenda haki kwa namna yoyote ile na mamlaka yoyote iwayo ni kichocheo cha amani kutoweka.  Viashiria vya upendeleo iwe ni upelelezi wa tukio la kutekwa, kuteswa na kutupwa msituni kwa Dk. Ulimboka kusuasua au kuachwa tu hivi hivi.


Upelelezi “fasta fasta” wa washukiwa wa mauaji ya kigogo wa Jeshi la Polisi, taarifa ya Kamati ya Serikali kuhusu mauaji ya Daudi Mwangosi, taarifa ambayo wakati ikisomwa kwenye runinga “body language” ya watoa taarifa iliwaonyesha wakihofia uwongo wao kuwasilishwa hadharani namna ile kwa wenye nchi yao -Watanzania; inaonyesha nchi yetu imefikishwa pabaya. Tafakari.

Arcado ni mmoja wa wanasiasa wakongwe nchini Tanzania . Ameshika nyadhifa mbalimbali zikiwamo za uwaziri katika wizara mbalimbali kuanzia Awamu ya Kwanza hadi Awamu wa Tatu. Anapatikana kupitia simu: 0787  617777