Habari kutoka Kenya zasema kuwa watu 34 wamefariki katika ajali nyingine mbaya ya barabani, iliyotokea mapema Jumapili asubuhi.

Watu 16 wamejeruhiwa wengi wao wakiwa katika hali mahututi, baada ya Basi moja la abiria kugongana ana kwa ana na lori la mizigo, katika maeneo ya barabara ya Sachangwan/ Salgaa, takriban kilomita 200 kutoka mji mkuu Nairobi.

Afisa mkuu wa idara ya polisi wa trafiki maeneo ya Bonde la Ufa, Zero Arome amesema ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa tisa alfajiri, kwenye barabara kuu ya kutoka Nakuru kuelekea Eldoret Magharibi mwa Kenya.

Shirika la msalaba mwekundu nchini Kenya limeandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Tweeter, kuhusiana na ajali hiyo ambapo mabaki ya magari hayo yaliyohusika kwenye ajali, yangali katika eneo la tukio, huku majeruhi wakipelekwa katika Hospitali za Nakuru Level Five na ile ya Molo Sub-County.

Mapema mwezi Disema zaidi ya watu 20 walifariki katika ajali maeneo hayo hayo.