Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (Forum on China-Africa Cooperation-FOCAC) utakaofanyika kuanzia Septemba 4 hadi 6, 2024 jijini Beijing, China.
Rais Samia anashiriki mkutano huo kufuatia mwaliko wa Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 31, 2024 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabiti Kombo amesema mkutano huo wa 9 wa FOCAC utafungulia na Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China ambapo, hotuba yake ya ufunguzi itatoa uelekeo wa China katika uhusiano wake na nchi za Afrika.
“Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo utaongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ataungana na Wakuu wa Nchi na Serikali wenzake kutoka Nchi zaidi ya 40 kati ya 54 za Bara la Afrika kushiriki Mkutano huo.
“Aidha, Antonia Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Moussa Faki, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika watashiriki Mkutano huo,” amesema.
Ameongeza kuwa, serikali ya China imemteua Rais Dkt. Samia kuhutubia kwenye hafla ya ufunguzi wa Mkutano huo wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa FOCAC itakayofanyika Septemba 5, 2024, akiiwakilisha Kanda ya Afrika Mashariki.
Amesema mkutano huo wa Kilele wa FOCAC utaongozwa na kauli mbiu isemayo ‘Kushirikiana ili Kuendeleza Usasa na Kujenga Jamii Bora ya China na Afrika kwa Mustakabali wa Pamoja ambayo inalenga kuwahamasisha Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika na China kujadili kuhusu masuala muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika na China ili kuongeza kasi ya maendeleo kwa pande zote mbili.
“Katika mkutano huo wa FOCAC Tanzania inatarajia kuwasilisha miradi mbalimbali ikiwemo mipya na ile ambayo haiweza kutelezwa kwenye mpango uliopita wa FOCAC kwa sababu mbalimbali, ili iweze kutekelezwa chini ya Mpango Kazi wa FOCAC kwa kipindi cha 2025-2027 kwa kupatiwa fedha za mkopo nafuu na msaada.
“Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Mtandao wa Mawasiliano Vijijini wa Awamu ya Pili, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa Kv 400 wa Awamu ya Pili na Tatu, ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) wa Awamu ya Pili pamoja na ujenzi wa barabara za Zanzibar zenye urefu wa Kilomita 277.7,” amesema.
Jukwaa la FOCAC lilianzishwa mwaka 2000 na Jamhuri ya Watu wa China kwa lengo la kukuza ushirikiano na maendeleo ya pamoja kati ya China na Afrika. Tangu kuanzishwa kwake jumla ya mikutano ya Kilele (Wakuu wa Nchi na Serikali) nane (8) imefanyika. Mikutano hiyo hufanyika kila baada ya miaka mitatu kwa kubalishana kati ya China na nchi moja ya Afrika.