Na Byarugaba Innocent, JamhuriMedia, Kibaha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ameridhia na kuidhinisha kiasi cha fedha shilingi Bilioni 3.9 kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha miundombinu kwenye Sekta ya Elimu,afya na Utawala Halmashauri ya Mji Kibaha kwa lengo la kutoa huduma stahiki kwa wananchi

Hayo yameelezwa na Afisa Masuuli ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Dkt.Rogers Jacob Shemwelekwa kwenye kikao Maalum cha kuweka mikakati ya kukamilisha Ujenzi kwa wakati alipoongea na Mafunzo 60 waliopewa kandarasi ya Ujenzi huku wakitarajia kutoa ajira zaidi ya 500.

Dkt.Shemwelekwa amesema kati ya fedha hizo Bilioni 2.9 ni bakaa ya Serikali kuu pamoja na wadau wa Maendeleo, Milioni 625.66 ni Mapato yanayokwenda kugharamia Miradi ya bakaa ya Mwaka wa fedha 2023/2024 na milioni 351.7 ni Mapato ya ndani yanayogharamia Miradi iliyopangwa kutekelezwa Mwaka huu wa fedha 2024/2025.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhe.Mussa Ndomba kando ya kumshukuru Rais wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia fedha hiyo, ametoa rai kwa Mafundi kufanyakazi kwa kuzingatia utalaam na uzalendo na kila mmoja atambue kuwa miradi hii itanufaisha watu wote hivyo malighafi zinazotakiwa zinunuliwe Kibaha ili kuinua uchumi wetu.

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe.Nickson Simon John amempongeza Dkt.Shemwelekwa kwa Mipango na mikakati kabambe aliyoweka kuhakikisha Miradi inakamilika ifikapo Novemba 20,2024 hivyo ametoa rai kwa Mafundi kufuata michoro, kuwa na mpangokazi itakayo waongoza kufanyakazi kwa matokeo.

Emmanuel Njovu, kwa niaba ya mafundi Ujenzi ameupongeza uongozi wa Kibaha Mji kwa kutoa kazi kwa wazawa na kwamba kitendo hicho kimeonesha namna wanavyo thamini utalaam wao na kuahidi kufanyakazi kwa uzalendo mkubwa

Miradi inayokwenda kujengwa na kukamilishwa ni shule 5 za Sekondari kupitia SEQUIP, kukamilisha mabweni,Kujenga Madarasa,Matundu ya vyoo,Ofisi za Mitaa, Hospitali ya Wilaya na Zahanati ili zianze kutoa huduma.

Dkt.Shemwelekwa amewaelekeza mafundi Kujenga Miradi yenye ubora unaoendana na thamani ya fedha, kuweka uwazi wa Matumizi ya fedha na malighafi,kuepusha malalamiko kwa vibarua na kukamilisha Miradi kwa wakati ili ianze kutoa huduma kwa Watanzania.