Na Lookman Miraji, JamhuriMedia,Dar ea Salaam

Mkuu wa wilaya ya kinondoni Saad Mtambule ameongoza mamia ya watu katika kampeni ya utunzwaji mazingira katika hafla iliyofanyika Asubuhi ya leo maeneo kunduchi, Dsm.

Kampeni hiyo ijulikanayo kama IRRIGATION TOUR imeratibiwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya ”Wise foundation ” ambayo inajihusisha na shughuli mbalimbali za mazingira na uwezeshwaji kwa wanawake .

Shughuli rasmi iliyofanyika leo hii ni kufuatuatilia maendeleo ya miti ambayo ilipandwa mnamo Februari 17, mwaka huu.

Akizungumza mapema leo hii wakati wa hafla hio Saad Mtambule alianza kwa kutoa pongezi za dhati kwa Taasisi ya Wise Foundation kwa kuandaa kampeni hiyo kwani itakuwa na faida nyingi katika jamii ya kitanzania ikiwemo kusaidia uhifadhi wa mazingira na kuongeza wimbi la ajira nchini.

Mbali na shukraan hizo Mtambule pia ametoa wito kwa wananchi wa wilaya ya kinondoni wote kuwa ajenda ya mazingira ni ajenda ya nchi nzima hivyo kuwaasa wananchi kutoacha barabara zikipigwa na jua na badala yake kuwa sehemu ya kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti na kuifanya wilaya ya kinondoni kuzungukwa na rangi ya kijani.

Aidha pia Mh Mtambule aliongeza kwa kuwasihi vijana kutumia fursa zilizopo katika upande wa mazingira bila kujali elimu walizonazo kwani fursa katika mazingira ziko wazi.

”Siku zote mahala panapokuwa na changamoto ujue kuna fursa pia zipo , hivyo tunapokuwa na changamoto kwenye upande wa mazingira pia kuna fursa unaweza ukaitumia ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira kutengeneza ajira, kutunza mazingira na kutengeneza kipato. Kwahiyo tutumie fursa hiyo vizuri bila kujali elimu gani umesoma tumieni muda wenu kuweka jitihada juu ya utunzwaji wa mazingira kwani kuna kuna wadau wengi kwenye mazingira fanya kitu fulani cha tofauti kwenye mazingira” alisema Mtambule.

Kwa upande wa Tasisi ya Wise Foundation kupitia mkurugenzi mkuu wa Taasisi hiyo Doricca Ambonisye akizungumza mara baada ya hafla hiyo kutamatika ambapo ameelezea kwa namna ambavyo wamefanikiwa kwa ukubwa katika kutekeleza kampeni hiyo ya umwagiliaji miti kwa mwaka huu.

Akizungumza Doricca amesema kuwa wamefurahi kuona wanaaminika na asasi mbalimbali za kiserikali na binafsi katika kushirikiana kuandaa kampeni hizo ambazo zimefanikiwa kupitia nguvu kubwa ya ushirikiano baina yao na taasisi hizo kwani isingekuwa rahisi kwa wao wenyewe kufanikisha kampeni hizo.

Aidha pia Doricca aliongeza kwa kuyaelezea malengo ya taasisi ya wise foundation ambayo ni kuhakikisha inatengeneza jamii inayotunza mazingira na kuyapa matokeo mazuri endelevu ya utunzwaji wa mazingira.

”Malengo makubwa ya wise foundation ni kuhakikisha tunakuwa na jamii inayotunza mazingira na sio tu kuyatunza bali pia kuyapa matokeo mazuri endelevu. Pia tuna malengo ya kuhakikisha vijana pamoja wanawake watanzania wanakuwa na mfumo bora wa maisha.

Mfumo bora wa maisha kwa maana ya kuwabadilisha kutoka kwenye wimbi la kuwa na watumiaji wengi zaidi ya wazalishaji, hivyo tumelenga kuijenga jamii itakayokuwa na wazalishaji wengi zaidi ya watumiaji kwasababu nia na rasilimali zote tunazo” alisema. .

Pia tukio liliambatana na zoezi la ugawaji wa tuzo ya shukraan kwenda kwa mkuu wa wilaya ya kinondoni Mhe; Saad Mtambule ambapo ametunikiwa tuzo hiyo kwa kuthamini jitihada na ushirikiano mkubwa anaotoa kwa taasisi ya wise foundation.
Mbali na tuzo hiyo tuzo nyingine zilienda kwa wadau kutoka taasisi mbalimbali ambazo zimetoa ushirikiano mkubwa katika kufanikisha kampeni hiyo.

Wataalamu wa mambo ya mazingira wanaielezea kampeni hiyo kama kampeni kamilifu kwa kuwa takriban asilimia 98 ya miti yote iliyopandwa mnamo februari 17 mwaka huu imestawi na kukuwa kama ilivyotegemewa.

Please follow and like us:
Pin Share