Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

ZAIDI ya wakulima 100,000 wameweza kushiriki kilimo ikolojia hai baada ya kupata elimu kupitia Mradi wa Jarida la Mkulima Mbunifu ambalo linatoka mara moja baada ya miezi miwili.

Hayo yamesema na Meneja Mradi wa Mkulima Mbunifu, Erica Rugabandana wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii mwisho mwa wiki.

Rugabandana amesema mradi huo wa Mkulima Mbunifu upo chini ya Shirika la BioVision Africa Trust kupitia Program ya Mawasiliano kwa Wakulima ambayo ina miradi mitano ambapo miradi minne ipo nchini Kenya na mmoja Tanzania ambao unasimamiwa na Shirika la Kilimo Endelevu Tanzania (SAT).

Amesema Mkulima Mbunifu kama mradi wanajishughulisha na kutoka jarida la kilimo ikolojia hai ambapo kunakuwa na makala mbalimbali zenye mbinu za kilimo hai, ufugaji wenye tija, lishe bora na utunzaji wa mazingira.

“Tunapozungumzia kilimo ikolojia hai ni kilimo ambacho kinahakikisha kwamba dhana nne ya kuhusu afya ya binadamu, mnyama, mazingira na mimea inayokuzwa inakuwa salama. Hivyo jarida linaandikwa katika kiswahili chepesi ambacho kinamuwezesha mkulima aweze kuelewa na kufanya kilimo hicho,” amesema.

Rugabandana amesema jarida hilo ambalo linatoka mara moja kwa miezi miwili linakuwa na tafiti na mbinu ambazo wakulima wanatumia kulima kilimo ikolojia hai.

Amesema mradi huo wa Mkulima Mbunifu kwa hapa nchini wanafanya kazi katika mikoa ya Manyara, Singida, Arusha, Kilimanjaro na Tanga, huku wakilisambaza katika vikundi mbalimbali vya wakulima nchini.

“Tumeweza kufikia wakulima zaidi ya 100,000 nchini Tanzania pamoja na mikoa niliyoitaja hapo juu, kwa vikundi ambavyo vimejisajili kwetu tunawatumia jarida hili na mwitikio ni mkubwa,” amesema.

Amesema wamekuwa wakipokea vikundi vipya vya wakulima wakitaka kupata jarida hilo na kwamba dhamira yao ni kufikia wakulima wengi zaidi nchini, kwani kilimo ikolojia kinaonekana kuwa suluhu za changamoto za kilimo.

Rugabandana amesema kila baada ya miezi mwili wanatoa nakala 15,000 na kila jarida moja linasomwa na watu watano hadi 10, ila pia wameweza kufikia zaidi ya watu 3,442 ambao wanapata taarifa za kilimo ikolojia hai.

Meneja huyo amesema wamefikia wakulima viongozi zaidi 53 ambao wamekuwa wakitoa elimu kwa wakulima wengine, hivyo kuleta mabadiliko chanya katika sekta hiyo.

“Tuna wakulima viongozi zaidi ya 53 ambao wamefanikiwa na wamekuwa wakifundisha wengine kupitia jarida hilo ambalo limelenga kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo,” amesema.

Rugabandana amesema lengo la jarida ni kuhakikisha wakulima wa Tanzania wanarejea katika kilimo ikolojia hai kwa kuwa hakina gharama, ni salama, mazao yanathamani kubwa, hakihitaji kununua mbegu kila wakati na mbolea yake ipo shambani.

Amesema mradi huo umekuwa ukitekelezwa kwa miaka mitatu, mitatu kufuatana na mfadhili ambae ni Biovision Foundation ya Uswisi. Hata hivyo wamejipanga kufikia wakulima wengi zaidi kupitia wadau washiriki katika maeneo mbalimbali.

“Tunataka kuhakikisha angalau asilimia 25 ya wakulima wanapata elimu ya kilimo ikolojia hai, hivyo tunawaomba wadau wengine kusaidia ili tuweze kutoa nakala nyingi za jarida hili,” amesema.

Aidha, Rugabandana ametaja changamoto ambazo wanakutana nazo kwenye kuandaa jarida ni wakulima kuuliza kuhusu masoko ya mazao yao, hivyo wamekuwa wakiwashauri wakulima kutafuta soko katika maeneo yao kwanza kabla ya kutafuta nje.

Pia ametaja changamoto nyingine ni asilimia kubwa ya maofisa ugani kukosa vitendea kazi vya kutosha ambavyo vinawawezesha kufikia wakulima kwa wakati.

Meneja huyo amesema wakulima wanatambua faida ya kilimo hicho, hivyo ni vema sekta husika kuwaunga mkono ili kuleta tija kwa nchi na wananchi.

Please follow and like us:
Pin Share