Serikali ishughulikie vurugu za kidini

Naungana na Watanzania wenzangu kulaani mauaji ya viongozi wawili wa dini ya Kikiristo yaliyotokea mkoani Geita na mjini Zanzibar, hivi karibuni. Aidha, natoa mkono wa tanzia kwa familia, ndugu na waumini wa dini hizo.

Mauaji hyo yamemfika Mchungaji Mathayo wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of God mkoani Geita, katika ugomvi wa kuchinja wanyama kati ya Waislamu na Wakiristo.

 

Padri wa Kanisa Katoliki Minara Miwili Zanzibar, Evarist Mushi, aliuawa kwa kupigwa risasi tatu kichwani na watu wasiojulikana wakati akishuka katika gari lake kwenda kuendesha ibada katika Kanisa la Mtakatifu Theresia eneo la Mtoni Zanzibar.


Mauaji hayo yameshitua, yametikisa na yamewasikitisha viongozi wa dini, Serikali na Watanzania wapenda amani na utulivu na wenye kuthamini ubinadamu. Ni matendo yanayoashiria uvunjifu wa amani na upotevu wa sifa nzuri ya Tanzania inayotambulika kama Kisiwa cha Amani. Vifo hivyo vimeamsha hisia kali, jazba na msisimko wa itikadi badala ya kutawaliwa na busara, amani, upendo na undugu kutoka kwa waumini wa dini, Serikli na viongozi wa siasa. Ni wakati mgumu uliojaa majonzi lakini hauna budi kuvumiliwa.


Lakini, tayari kiongozi mmoja wa dini amekaririwa na gazeti moja litokalo mara moja kwa wiki (si JAMHURI), akionya kuwa Wakristo wakiona vurugu na mauaji dhidi yao yakishamiri wataingia mitaani na kuwafanyia fujo Waislamu, na amani haitakuwapo tena.

 

Amekwenda mbali zaidi kwa kusema; “Huu sasa ni wakati wa jeshi letu kuingia mitaani na kuhakikisha kikundi hicho kinaondolewa mara moja kabla hatujawa kama ‘Nigeria’.

 

Kiongozi huyo amesema hivyo kwa sababu ana uchungu wa kufiwa na kuhisi kuonewa. Namuomba apige moyo konde na amwachie Mwenyezi Mungu muweza wa kila jambo, atatoa hukumu.


Nampa pole Polycarp Kardinali Pengo kwa kufiwa na mtendaji wake Padre Mushi. Pokea mkono wa tanzia. Pili, nakubali busara iliyotolewa na Kardinali Pengo ya kuwataka Wakristo wasilipize kisasi. Wakilipiza amani haitakuwapo.


Aidha, ametaka Serikali iache tabia ya kupuuzia matukio kama hayo ya hatari; kuchukua hatua haraka yanaposikika au yanapotokea.


Ni kitambo sasa nchi yetu imeingiliwa na sera za chokochoko katika mikakati ya kuvunja amani na utulivu nchini kwa visingizio vya demokrasia na utawala bora, imani za dini na uchumi unaobeba uwekezaji wa rasilimali za nchi.

 

Wananchi wanashuhudia malumbano ya matamko kinzani na dharau kutoka kwa wanasiasa. Kejeli na kashfa zinaporomoshwa na waumini wa dini tofauti na vikundi vya uporaji rasilimali unaofanywa na wawekezaji dhidi ya wananchi.


Matendo hayo yamekwisha kusababisha vurugu zilizozaa majeruhi ya watu na wengine kuuawa. Kulaumiana na kutuhumiana kunachukua nafasi ya undugu na upendo, uaminifu na utulivu ndani ya jamii ya Watanzania.


Lazima Watanzania wakae pamoja na kujiuliza huu utaratibu au utamaduni wa kutukanana, kupigana na kuuana unatoka wapi? Watanzania mkubali kinyegere ameingia nchini anaua watu. Mshike magongo kumsaka, kumkamata na kumuua, ama sivyo nchi itaangamia.


Nashauri wakati wa kuwasaka na kuwakamata vinyegere uangalifu na uadilifu utumike ili usaliti, ulaghai na uhaini usitokee. Mambo kama hayo yamekwishatendeka katika mataifa kadhaa Afrika kama vile Somalia, Mali, Nigeria, Libya na DR-Congo.


Ni vyema na busara vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vikaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ujasiri, uzalendo na uadilifu kuimarisha na kuboresha zaidi mafunzo ya vyombo hivyo, kuliko kuingiza vyombo vingine kutoka nchi za nje, hasa za Magharibi. Tutaangamia!

 

Nasema ni busara vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kutumika kwa sababu, “msingi wa maendeleo ya ulinzi na usalama wa Tanzania ni Watanzania wenyewe, kila Mtanzania, na hasa kila mzalendo na kila mjamaa.” (mwongozo wa TANU, 1971).


Jeshi la Polisi liendelee kutekeleza jukumu lake vizuri kuwapatia wananchi na hasa vijana, mafunzo juu ya ulinzi shirikishi ili wawe tayari kulinda katika maeneo yao, kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, 2005 na 2010.


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiendelee kuisukuma Serikali yake kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010, inayotaka halmashauri za majiji kuanzisha vikosi rasmi vya usalama wa raia ili kuimarisha ulinzi katika maeneo hayo.


Nakamilisha makala yangu kwa kuungana na Watanzania wanaotaka Serikali kuitisha mijadala ya kitaifa ya makundi ya dini zote nchini, kusikiliza malalamiko yao na kutoa uamuzi. Mijadala hiyo itabaini vyanzo vya migogoro na malalamiko yaliyopo.

Mungu ibariki Tanzania.