Na Stella Aron, JamhuriMedia, Harare Zimbabwe

Tanzania inashiriki kikamilifu juhudi za kutafuta amani ndani ya kanda, barani Afrika na duniani ikiwa ni pamoja na kuchangia gharama zake.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo nchini Zimbabwe katika mkutano wa Kamati Asasi ya Ushirikiano ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO)

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) akishiriki Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) uliofanyika Harare, Zimbabwe tarehe 16 Agosti, 2024.

Waziri Kombo amesema Tanzania inalipa kipaumbele suala la kuimarisha ulinzi na usalama katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

“Katika kufanikisha hili Tanzania inashiriki kikamilifu juhudi za kutafuta amani ndani ya kanda, barani Afrika na duniani ikiwa ni pamoja na kuchangia gharama zake” amesema.

Ameongeza kuwa Tanzania inaamini kuwa uzoefu wake utaiwezesha kuchangia kwa ufanisi katika jukumu la Baraza la Usalama.

Kushoto ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (MBW) wakifuatilia Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) uliofanyika tarehe 16 Agosti, 2024.

Waziri Kombo pia amewasilisha ombi la Tanzania kuendelea kuungwa mkono na nchi za SADC katika nafasi mbalimbali zinazowaniwa na Watanzania ikiwemo nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) – Afrika inayowaniwa na Dkt. Faustine Ndugulile.

Katika hatua nyingine ameomba Tanzania kuungwa mkono katika nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha mwaka 2026 – 2028 na Ujumbe usio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha mwaka 2029 na 2030.

Mkutano huo ulitanguliwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu uliofanyika kuanzia Agosti 15, 2024 ambapo, mikutano hii miwili ni ya awali ya maandalizi ya agenda na nyaraka kwa ajili ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika leo tarehe 16 Agosti, 2024 ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan atateuliwa kuwa Mwenyekiti wa asasi hiyo.

Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo akifuatilia Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) uliofanyika tarehe 16 Agosti, 2024 Harare Zimbabwe.  

Agenda zilizojadiliwa na mkutano huu ni pamoja na Hali ya Ulinzi na Usalama katika Kanda, Uimarishwaji wa Demokrasia katika Kanda, Mfumo wa Kuwaenzi Viongozi Waasisi wa SADC na Wagombea wa Nafasi mbalimbali wa Kanda katika Jumuiya za Kikanda na Kimataifa.

Mkutano huo pia umehudhuriwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya ya Rais – Ikulu, Zanzibar, Mhe. Ali Suleiman Ameir (MBW).

Kulia ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Jacob Mkunda akifuatilia Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) uliofanyika Harare, Zimbabwe tarehe 16 Agosti, 2024.
Please follow and like us:
Pin Share