Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga

CHANGAMOTO ya uhaba wa mashine za kuchakata Mkonge (korona) inayowakabili wakulima katika maeneo yao inatarajiwa kuwa historia hatua itakayochochea ongezeko la uzalishaji wa zao hilo.

Hatua hiyo imetokana na ziara ya Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), ambao walitembelea miradi mbalimbali ikiwemo mashamba ya Vyama vya Ushirika na Masoko (Amcos) na viwanda vya uchakataji Mkonge mkoani Tanga kubaini moja ya changamoto kubwa inayowakabili wakulima ni uchache wa mashine hizo kulingana na mahitaji.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Theobald Sabi amesema pamoja na mambo mengine ziara iliyolenga kujionea Sekta ya Mkonge kuanzia kwenye mashamba hadi uchakataji na kuelewa kwa ujumla mnyororo mzima wa thamani wa sekta hiyo lakini pia changamoto zinazowakabili wakulima na wote waliopo kwenye sekta ndogo ya Mkonge.

“Nia yetu ni kuhakikisha kwamba tunapata suluhisho la changamoto ambazo zimekuwapo hasa kwenye eneo la uchakataji mkonge. Tumejionea mashine ambazo zinafanya vizuri na zile zenye changamoto tutachukua hatua kama bodi kuhakikisha kwamba shughuli nzima za Mkonge zinakwenda vizuri ili tujenge tija kwa wakulima, mamlaka, bodi, uchumi na pato la taifa kwa ujumla,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TSB, Saddy Kambona amesema licha ya ziara hiyo ya kujifunza na kujenga uelewa lakini jambo kubwa ambalo walitaka kujionea ni kukosekana kwa mitambo ya uchakataji Mkonge na kupata majawabu kwa wakulima juu ya namna ya kuondokana na changamoto hiyo.

“Kwa hiyo tuliwapitisha maeneo mbalimbali lakini pia tukawaonesha jitihada ambazo sisi kama bodi au menejimenti tumezichukua kuondoa hiyo changamoto ya uchakataji ukiondoa jitihada ambazo tunaendelea nazo kupitia wizara yetu ya kilimo ya mipango ya serikali kununua mitambo ya uchakataji na kuiweka maeneo mbalimbali.

“Lakini pia tuchukue nafasi nyingine kuwakaribisha wawekezaji binafsi kuwekeza mitambo kwenye mashamba hapa Korogwe ili kujaribu kupunguza changamoto za uchakataji ambazo zimekuwa zikilalamikiwa mara kwa mara,” amesema na kuongeza:

“Leo wakurugenzi wamejionea tofauti iliyopo kati ya mitambo ambayo imekuwepo miaka yote ambayo imekuwa ikiendeshwa na Sisalana lakini na ile mitambo mipya ambayo imewekezwa na wawekezaji binafsi ikiwamo Hale na Magunga hatua hiyo imesaidia kupunguza changamoto ya uchakataji kwa wakulima katika maeneo yao,” amesema Mkurugenzi Kambona.

Aidha, amesema Menejimenti inategemea baada ya ziara hiyo watakapokutana kwenye kikao cha bodi watapokea maelekezo mbalimbali baada ya wakurugenzi kujionea hali halisi kwenye hizo Amcos na uchakataji unavyokwenda.

“Tunategemea watatupa miongozo na maelekezo kama menejimenti tunaahidi kutekeleza yale yote tutakayoelekezwa kuhusiana na namna mbalimbali ya kutatua changamoto hii ili kufikia malengo ya kuzalisha tani 120 kwa mwaka ifikapo 2025,” amesema Kambona.

Naye Mjumbe wa Bodi hiyo, Naweed Mullah, amesema katika ziara hiyo wamejionea mazuri mengi ambapo ametoa wito bodi kuangalia namna watu wa uchakataji waongezeke lakini pia waangalie namna ya kutoa huduma ili kuwe na bei nafuu.

“Wakulima wamehamasika inafurahisha kuona yako mashamba mengi yanaandaliwa lakini wanaangushwa kidogo kwenye mambo ya usindikaji na usimamizi wote ndani ya mfumo huo. Wito wangu ni wanaoshiriki kwenye biashara hiyo wajitahidi kutoa huduma bora mashine ziwe zinahudumiwa kwa wakati ili wananchi wanufaike na miradi hiyo,” amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Magunga Amcos na Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Amcos za Mkonge Tanga, Shedrack Lugendo ameishukuru bodi kuwatembelea na kujionea shughuli wanazofanya na kuongeza kuwa mitambo ya uchakataji Mkonge ya Kampuni ya Sisalana imepitwa na wakati na hazina matengenezo mazuri ambapo mkonge mwingi unaishia kwenye mtaro mkulima anapata hasara.

“Kwa hiyo tuna matarajio makubwa kwa hizi Amcos tano kwa kuwa Bodi ya Wakurugenzi imepita na Amcos zimeomba kuwekeza viwanda na kila kitu tulishamaliza kwa hiyo tunaamini baada ya ziara hii tunachowaomba waharakishe Amcos ipate korona zake ili iwe mkombozi kwa wakulima,” amesema.

Please follow and like us:
Pin Share