Jeshi la Polisi linapenda kutoa taarifa kwa umma kuhusiana na kuwepo kwa mipango ya viongozi wa chama cha siasa nchini [CHADEMA] kuhamasisha vijana kote nchini kukusanyika Mkoa wa Mbeya Agosti 12, 2024 kwa lengo la kufanya maandamano na mikusanyiko kwa mwamvuli wa maadhimisho ya siku ya vijana duniani.

Hivi karibuni kupitia mitandao ya kijamii wameonekana na kusikika baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo [CHADEMA] wakihamasisha vijana kote nchini, viongozi wa kitaifa wa chama, kamati kuu ya chama hicho na kualika baadhi ya watu kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kwenda kuadhimisha siku ya vijana Mkoani Mbeya.

Pamoja na mwaliko wanaotoa, viongozi hao wameendelea kutoa kauli ambazo hazionyeshi kuwa na lengo la kwenda kuadhimisha siku ya vijana duniani bali ni kwenda kuhamasisha kufanya vitendo vinavyolenga uvunjifu wa amani kwa wananchi wa Mkoa wa Mbeya.

Miongoni mwa kauli hizo ambazo zinaashiria kuwa na lengo la kuvuruga amani ni za Katibu Mwenezi BAVICHA Taifa ndugu Twaha Mwaipaya, nanukuu “Kama kijana yeyote unaipenda nchi yako ya Tanzania, umeshalia miaka yako yote, siku hiyo ya tarehe 12/08/2024 tunakwenda kuweka hatma ya Taifa letu la Tanzania Mkoani Mbeya, kwa hiyo kijana yeyote uliyepo popote Tanzania njoo uwanja wa Ruanda Nzovwe Mbeya”

Kauli nyingine ni, “Tupo serious sana na jambo hili, kwa hiyo vijana wote wa CHADEMA kama ambavyo vijana wa Kenya wamejitambua, siku ya tarehe 12/08/2024 tunakwenda kuacha uteja kwa serikali vijana wa kitanzania na kuweka maazimio makubwa ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2025”

Kauli zinazotamkwa kama hizi za kwamba wanakwenda kuamua hatma ya Taifa la Tanzania na kwamba wapo “serious” sana kama ambavyo vijana wa Kenya walijitambua na kuacha uteja wa serikali na taarifa zingine zilizopo ni viashiria tosha kuwa malengo yao sio kwenda kuadhimisha siku ya vijana duniani bali ni kuanzisha na kufanya vurugu ili kusababisha uvunjifu wa amani nchini.

Kufuatia kauli hizo na matamko mbalimbali yanayotolewa na viongozi hao, Jeshi la Polisi limeamua kupiga marufuku maandamano na mikusanyiko ya aina yoyote ile ya ndani au nje inayotaka kufanyika kwa mwamvuli wa kuadhimisha siku ya vijana duniani inalenga kuleta uvunjifu wa amani Mkoa wa Mbeya na maeneo mengine yoyote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo basi, Jeshi la Polisi nchini linatoa onyo kali na katazo kwa mtu au kikundi cha watu kinachojipanga kufanya maandamano na mikusanyiko kuacha mara moja kwani Jeshi la Polisi lipo imara na limejipanga vizuri kuhakikisha ulinzi, usalama, amani na utulivu vinatawala nchini na lipo tayari kuzuia na kupambana na viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani, na halitasita kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria kwa mtu yeyote atakayekiuka katazo hili.

Please follow and like us:
Pin Share